JESHI la Polisi mkoani Songwe limewakamata watu wawili kwa tuhuza za kukutwa wakitengeneza noti bandia za nchini Zambia. Anaripoti Ibrahim Yassin, Songwe…(endelea).
Akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 3 Oktoba 2023, Kamanda wa polisi mkoani Songwe, Teopista Malya amesema watuhumiwa hao wamekamatwa leo mchana katika mtaa wa Nazareth kata ya Mwakakati halmashauri ya mji Tunduma wilayani Momba mkoani hapa.
Bila kuwataja majina watuhumiwa, Kamanda Malya amesema mtuhumiwa mwenye umri wa miaka 48, ni mkazi wa Mpulungu Zambia na wa pili (49) mkazi wa Msongwa Tunduma. Wote wamekutwa na noti 12 za Kwacha zenye thamani ya Kwacha 50 za nchini Zambia.
Aidha, Kamanda Malya amesema watuhumiwa hao pia walikamatwa na karatasi 10 za ukubwa wa A4 zilizochapishwa kwacha 50 kwa idadi ya noti bandia 36 kwenye karatasi hiyo ambayo pia ilichapishwa noti 4 zenye thamani ya kwacha 100 zenye namba EJ228951989 na EJ220684457 na EJ17714847.

Amesema pia waliwakamata wakiwa na visu viwili, mkasi wa kukatia karatasi, vitambulisho viwili vya Taifa la Zambia, vyenye namba Z.7714847 na Z,1600353.
Hata hivyo, amesema jeshi hilo linaendelea kufuatilia mtandao mzima wa kundi hilo la kutengeneza noti bandia na kwamba waliokamatwa watafikishwa mahakamani pindi uchunguzi utakapokamilika.
Leave a comment