WATU wanaopewa fedha na wapenzi wao kwa ajili ya matumizi mbalimbali, wametakiwa kutunza kumbukumbu ili kutojiweka katika hatari ya kufunguliwa kesi za uhujumu uchumi na utakatishaji fedha. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).
Wito huo umetolewa leo tarehe 5 Aprili 2024 na Wakili kutoka Kampuni ya Mawakili ya Afritanza, Onesmo Olengurumwa.
Wakili Olengurumwa amesema kuna baadhi ya watu wamejikuta wakikabiliwa na changamoto hiyo kutokana na kutoweka kumbukumbu za miamala ya fedha wanazotumiwa au kutuma kwa wengine, kitendo ambacho ni kinyume cha Sheria.
“Ni Kosa Kisheria kuwa na Miamala ya fedha isiyokuwa na maelezo kuwa imetoka kwa nani na kwa ajili gani imekuja kwako. Hakikisha kila hela unayopata unajua vizuri chanzo chake na pia kuweka kumbukumbu sawa umepokea kwa ajili ya nini.
“Kama ni kazi umefanya au biashara hakikisha kodi stahiki zimelipwa, kama ni hela ya msaada weka kumbukumbu sawa imetoka wapi na kwa ajili ya nini. Kutokuzingatia haya utajiweka katika hatari ya makosa ya kodi , utakatishaji fedha na uhujumu uchumi,” amesema Wakili Onesmo Olengurumwa.
Wakili huyo amesema “mfano kule Kenya kuna mwanamke alitumiwa fedha Dola 1,000,000 na mpenzi wake bila maelezo ya kutosha zikataifishwa. Kuna katibu tawala wa wilaya juzi alikuwa na kesi ya utakatishaji milioni moja na nusu sababu hazikuwa na maelezo.”
Wakili Olengurumwa amesema, hata kama umetumiwa kiasi kidogo cha fedha bila maelezo yake, mtu anaweza kuingia matatani.
“Watu wengi wanatumiana hela toka nje au ndani ya nchi , hata kama unatuma hela kwa mzazi au mtoto au mke hakikisha unaweka rekord vizuri ili kumlinda mpokeaji wa hela hizo endapo huko mbele zitakuja kuonekana hazina ushahidi zilitoka wapi- Nashauri tujenge kuweka kumbu kumbu vizuri ya hela tunazopokea toka sehemu mbalimbali aidha kwa simu kwa bank au kwa njia nyingine,” amesema Wakili Olengurumwa.
Leave a comment