May 20, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wanaharakati ‘wawaangukia mawakili wanawake

Onesmo Olengurumwa, Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC)

Spread the love

 

WATETEZI wa haki za binadamu nchini Tanzania, wametoa wito kwa mawakili wanawake kuwa mstari wa mbele katika kushughulikia kesi zinazohusu maslahi ya umma, hasa kutetea haki za binadamu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Wito huo umetolewa kwenye mjadala wa kuwajengea uwezo wanawake katika kusimamia kesi zinazohusu maslahi ya umma, uliofanyika jana tarehe 6 Machi 2021, kupitia mtandao.

Mjadala huo uliratibiwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TWLA).

Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa alisema Tanzania inakabiliwa na ombwe la mawakili wanawake wanaotetea kesi hizo.

“Katika mawakili waliosajiliwa wanawake na wanaume karibu wako sawa, idadi yao inakaribia nusu kwa nusu, lakini trend inaonesha waliokuwa mstari wa mbele kutetea mashtaka ya umma ni wanaume, idadi ya wanawake ni ndogo,” amesema Olengurumwa.

Olengurumwa amesema semina hiyo ililenga kuwajengenea uwezo mawakili wanawake, ili waweze kushiriki katika kesi zinahusu utetezi wa haki za binadamu.

“Kuelekea siku ya mwanamke duniani tunahitaji kukaa nao, tuwajengee uwezo ili tuongeze idadi ya mawakili wanawake katika mashauri yanayohusu masilahi ya umma,” amesema Olengurumwa.

Mgeni rasmi katika semina hiyo, Jaji wa Mahakama Kuu Tanzania, Lilian Mongela aliwaomba mawakili wanawake kutumia uzoefu wao kushiriki katika kesi hizo.

“Wanaoshiriki katika kesi za masilahi ya umma kama ardhi, ajira na wafanyakazi, mchango wa wanawake ni mdogo. Mawakili waliosajiliwa Tanzania wanawake wako 3,055, lakini wanaoshiriki katika kesi zinazohusu masilahi ya umma ni wachache. Mawakili wanawake wanapswa kushiriki katika kesi hizo kwa kuwa wanaweza kama wanavyofanya vizuri katima kesi nyingi,” alisema Jaji Mongela.

Kwa upande Wakili Najutwa Sengondo, alisema kinachowakwamisha kutetea kesi zinazohusu utetezi wa haki za binadamu, ni changamoto mbalimbali wanazokutana nazo.

Alitaja changamoto hizo kuwa ni, uhaba wa rasilimali fedha na mafunzo kuhusu usimamiaji kesi zinazohusu masilahi ya umma.

“Kinachosababisha ni ukosefu wa raslimali na mazingira ya sasa yalivyo. Kama unavyoona baadhi ya wanaharakati wanaume wanavyokabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kukamatwa. Hii inatisha watu mawakili wanawake na kuwafanya warudi nyuma,” alisema Wakili Sengondo.

error: Content is protected !!