Friday , 3 May 2024
Home Habari Mchanganyiko Wahariri kufundwa uhifadhi wa bioanuwai
Habari Mchanganyiko

Wahariri kufundwa uhifadhi wa bioanuwai

John Chikomo
Spread the love

CHAMA cha Waandishi wa Mazingira Tanzania (JET) kwa kushirikiana na USAID Tuhifadhi Maliasili wameandaa mafunzo kwa wahariri 25 wa vyombo vya habari kuhusu uhifadhi wa bioanuwai. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa JET, John Chikomo wakati akizingumza na MwanaHALISI Online kuhusu mikakati ya taasisi hiyo katika kuhifadhi bioanuwai.

Chikomo alisema Tanzania ni moja ya nchi zenye bioanuwai nyingi duniani, ikiwa na spishi zaidi ya 55,000 ikiwa ni theluthi moja ya spishi za mimea na asilimia 20 ya spishi kubwa za wanyama barani Afrika.

“Kwa bahati mbaya, katika miongo kadhaa iliyopita, Tanzania imepoteza theluthi moja ya mifumo muhimu ya ikolojia na kushuhudia kupungua kwa idadi ya spishi na ukubwa wa idadi yao. Katika muongo uliopita pekee, idadi ya spishi zilizo hatarini nchini Tanzania imeongezeka mara tatu,” alisema.

Alisema moja ya changamoto katika uhifadhi wa bioanuwai ni ukosefu wa data, elimu na mtiririko wa taarifa mfumo kuhusu upotevu wa bioanuwai na thamani ya kiuchumi ya bioanuwai, hivyo ni muhimu wahariri kupata elimu.

“Changamoto za uhifadhi kama vile spishi za kigeni na mabadiliko ya hali ya hewa katika njia za wanyamapori na maeneo ya hifadhi yanahitaji jitihada za pamoja za wadau wa uhifadhi ili kuzitatua,” alisema.

Alisema USAID Tuhifadhi Maliasili kwa kushirikiana na JET wameandaa mafunzo ya siku mbili wa wahariri, ili kuunda jukwaa la mwingiliano kati ya waandishi wa habari na wataalamu wa uhifadhi ikiwa na lengo la kuongeza maarifa na kuhamasisha ufahamu miongoni mwa raia wa Tanzania kuhusu uhifadhi wa bioanuwai.

“Mafunzo kwa wahariri ni moja ya mikakati ya kuongeza ubora na wingi wa taarifa za uhifadhi wa bioanuwai katika vyombo vya habari, ili kuleta mabadiliko na mitazamo miongoni mwa Watanzania kuhusu uhifadhi na kupata habari sahihi kwa ajili ya kuripoti,” alisema.

Chikomo alisema program hiyo ya mafunzo imeanza na wahariri kutoka vyombo vya Daily News, Nipashe, The Citizen, Tanzania & Beyond Magazine, Raia Mwema, BEST Media, Clouds Radio/TV, The Guardian, TBC Taifa,  Mwananchi, HabariLeo, ITV na TBC.

Alisema wahariri hao wataweza kuongeza maarifa kuhusu masuala ya uhifadhi wa bioanuwai, ili kuripoti vizuri, kuelimisha umma wa Tanzania, kuwahusisha waandishi wa habari na wataalamu na wadau muhimu wa bioanuwai kwa ajili ya kuripoti siku za usoni.

Mkurugenzi huyo alisema kupitia mafunzo hayo waandishi wataongezewa maarifa, kuongezeka kwa ubora na wingi wa hadithi katika vyombo vya habari na kuongezeka kwa ufahamu miongoni mwa umma wa Tanzania kuhusu uhifadhi wa bioanuwai.

Aidha, alisema mafunzo hayo yatajadili changamoto za spishi za kigeni katika uhifadhi na maendeleo ya jamii, jukumu la Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA) katika kupambana na uhalifu wa wanyamapori na kukuza utalii nchini Tanzania.

Pia watajadiliana uhamasishaji juu ya migogoro kati ya binadamu na wanyamapori na suluhisho ambazo zimefanikiwa na zisizofanikiwa, jinsi vyombo vya habari vinavyoripoti migogoro kati ya binadamu na wanyamapori.

“Vyombo vya habari vina jukumu kubwa katika kuchochea maendeleo ya kitaifa kwa kuripoti kwa uwazi taarifa za umma na kuhakikisha wale wenye madaraka wanawajibika,” alisema.

Chikomo alisema mkutano huo wa wahariri utachambua ubora wa kuripoti wa vyombo vya habari kuhusu maeneo ya uhifadhi wa bioanuwai na taarifa nyingine za uhifadhi nchini kwa kutumia uzoefu kutoka kwa wahariri, wablogu, na wadau wa vyombo vya habari.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoTangulizi

Kimbunga “HIDAYA” chaendelea kuimarika, wananchi wapewa tahadhari

Spread the loveMAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kutoa taarifa...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Chadema waendelea kulilia katiba mpya

Spread the loveCHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeendelea kudai upatikanaji wa...

BiasharaHabari Mchanganyiko

NMB yang’ara maonesho OSHA

Spread the loveBenki ya NMB imebeba tuzo ya kampuni bora kwenye sekta...

Habari MchanganyikoKimataifa

Ruto amteua Kahariri kuwa mkuu wa majeshi

Spread the loveRAIS wa Kenya, William Ruto, amemteua Jenerali Charles Muriu Kahariri,...

error: Content is protected !!