Tuesday , 18 June 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Wagombea ubunge CCM, presha inapanda, presha inashuka
Habari za SiasaTangulizi

Wagombea ubunge CCM, presha inapanda, presha inashuka

Spread the love

TAKRIBANI wanachama 8,000 kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), walioshiriki mbio za ubunge kupitia chama hicho, sasa wako matumbo joto, kufuatia kuibuka kwa taarifa, kwamba “lolote linaweza kutokea.” Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Taarifa kutoka ofisi ndogo ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam na Dodoma zinasema, hofu ya lolote linaweza kutokea, imetokana na kuwapo na madai kuwa kati ya wote walioshiriki kura za maoni, ni kidogo mno waliokuwa hawakujihusisha na vitendo vya rushwa.

Kiongozi mmoja mwandamizi wa chama hicho tawala ambaye hakupenda kutajwa jina lake amesema, “hawa walioshiriki kura za maoni za ubunge wako matumbo joto, wakihofia kuteuliwa kupeperusha bendera ya chama chao katika uchaguzi mkuu wa Oktoba.”

Anasema, “hii inatokana na chama kutumia kikamilifu kamati zake za maadili kushughulikia taarifa zote za uvunjifu wa maadili, ikiwamo madai kuwa baadhi ya wagombea walijihusisha na vitendo vya rushwa.”

Hofu kwa watiania hao wa ubunge, inatokana na taarifa za malalamiko kutoka miongoni mwao kuziwasilisha kwa viongozi wa chama hicho kuhusu kukithiri kwa vitendo vya rushwa wakati wa mchakato huo.

Samia Suluhu, Makamo wa Rais wa Tanzania ambaye pia ni Mgombea mwenza kwa tiketi ya CCM, akizungumza katika mkutano wa UWT

Tayari vikao vya mapendekezo ya jimbo, wilaya na mikoa vimekwisha fanyika na kinachosubiriwa sasa, ni vikao vya uteuzi vya Kamati Kuu (CC), ambavyo vinatarajiwa kufanyika muda wowote kutoka sasa.

Aidha, katika mitandao kadhaa ya kijamii, ikiwamo magroup songosi ya What App, kumesambazwa video na sauti za baadhi ya wagombea hao, wakizungumzia vitendo vya rushwa.

Kupatikana kwa taarifa kuwa baadhi ya wagombea wa ubunge, wakiwamo wabunge wanaomaliza muda wao, kwamba wametumia mlungula kutafuta ushindi, kumekuja katika kipindi ambacho, viongozi wakuu wa CCM wamejiapiza kuwa kila aliyejihusisha na rushwa, ataondolewa kwenye kinyang’anyiro hicho, hata kama alishinda.

Kura hizo za maoni, zimeshuhudia wabunge waliomaliza muda wao ambao walikuwa wakitetea nafasi hizo wakishindwa kufurukuta na kujikuta ama wakiwa nafasi ya pili na wengine wakishika nafasi ya nne.

Furaha Dominic Jacob

Vikao hivyo vya uteuzi vya CCM vinafanyika kipindi ambacho malalamiko yako mbele yake juu ya vitendo vya rushwa na kukiwa na makalipoa yaliyotolewa kwa nyakati tofauti na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hichi, Humphrey Polepole.

Viongozi hao, wamenukuliwa wakisema, wale wote waliojihusisha na vitendo vya rushwa majina yao yatawekwa kando ili kuhakikisha wanapata wagombea safi ambao hawajajihusisha na vitendo vya rushwa.

Mmoja wa mtiania katika jimbo la Kawe jijini Dar es Salaam aliyezungumza na mwandishi wa habari hizi anasema, “CCM ni ile ile. Rushwa ili kuwa nje nje na hata ukiangalia mazingira yalivyokuwa.”

Anasema, “najua chama kina taarifa zote, kwa sababu wajumbe waliokuwa wakishawishiwa wanajulikana na chama kina mtandao, kama kitafumbia macho hiko kilichojitokeza Kawe na maeneo mengine, chama kinaweza kuwa na wakati mgumu kwenye uchaguzi.

Juzi Jumatatu, Mama Samia Suluhu, makamu wa rais wa Jamhuri ya Muungano na Mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya CCM, alieleza kuwa chama chake kina taarifa za kila aliyegombea nafasi ya ubunge wa jimbo na ule wa viti maalum.

Mama Samia alitoa kauli hiyo, wakati akifungua mkutano wa Baraza Maalum la Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) jijini Dodoma. Mkutano wa UWT, ulikuwa mahususi kupigia kura za maoni kwa wabunge wa umoja huo.

Alisema, “nataka niwaambie, kama mlitoa rushwa tutakapo kaa vikao vya juu, mnamuelewa mzee wa mafaili. Kila mmoja tuna taarifa zake.”

Kauli hiyo ya Samia ilifanana na ile aliyoitoa siku moja kabla yaani Jumapili wakati akizindua jengo la ofisi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wilaya ya Mpwapwa jijini Dodoma, kwamba taasisi hiyo kushughulikia vilivyo vitendo vya rushwa.

Alisema, rushwa imekuwa mwiba kwa baadhi ya mawakala au wagombea kwenye uchaguzi ndani ya vyama kwa kutoa rushwa ili wapigiwe kura na baadhi ya wajumbe kuomba kura kwani matukio hayo si ya kiungwana na yanarudisha nyuma maendeleo.

“Sisi Chama Cha Mapinduzi, tunaendelea na mchakato wa kuwachambua viongozi na watakaobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa, tutawakata na msemo wa Rais huwa anasema kata na msemo huu utatumika kuangalia nani ni nani,” alisema Mama Samia.

Wakati Mama Samia akitoa kauli hiyo, Polepole akizungumza na waandishi wa habari 5 Agosti 2020 alisema, uchaguzi wa CCM unaongozwa na katiba na kanuni na kuzuia yale yote ambayo wameyazuia yasifanywe na unyenyekevu wa viongozi wakati wote wa mchakato.

Humphrey Polepole, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM

“Ifahamike wanaCCM wote tuko vizuri sana, napenda kuwahakikishia tuko vizuri sana na wale wachache ambao wamejaribu kutujaribu, tutawashangaza nasema tutawashangaza. Tunataka viongozi waadilifu, wachapa kazi na wanaochukizwa na rushwa na kwetu rushwa inakakatazwa, ” alisema Polepole.

“Wale mliopiga mazonge tutawafundisha adabu kipindi hiki. Sababu ukifundishwa adabu ni vizuri tukupe suprise ukapate kazi nyingine sababu uongozi unaotweza katiba yetu hauna nafasi,” alisema Polepole.

Muwe watulivu sababu nyie Watanzania wanawaamini kwenye wigo wa uongozi tulieni. Hatutawaangusha watu wanyenyekevu kwenye chama chetu muwe na amani.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Mazingira magumu ya JPM yamechangia ‘Comedy Journalism’

Spread the loveMwenyekiti wa Kamati ya kufuatilia hali ya uchumi wa vyombo...

Habari MchanganyikoHabari za SiasaTangulizi

RC Chalamila: Nimeacha ubabe

Spread the loveMKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chamalila amemthibishia...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Rais Samia atoa ujumbe mzito Sikukuu Eid Al Adha

Spread the loveKATIKA kusherehekea Sikukuu ya Eid Al Adha, Rais wa Tanzania,...

BiasharaHabari za Siasa

Dk. Biteko aipongeza NMB kwa kuanzisha utoaji wa bima ya mifugo

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko...

error: Content is protected !!