Friday , 3 May 2024
Home Kitengo Biashara Wafanyabiashara wamuanguakia Samia wasiondolewe Bandari kavu Jimbiza
Biashara

Wafanyabiashara wamuanguakia Samia wasiondolewe Bandari kavu Jimbiza

Spread the love

WAFANYABIASHARA katika Bandari Kavu ya Jimbiza, iliyoko Kilwa Masoko, mkoani Lindi, wameiangukia Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan wakiitaka iingilie kati ili wasiondolewe kwenye eneo hilo kumpisha mwekezaji Kampuni ya Kilwa Yark Club, wakidai  amekabidhiwa kinyume cha sheria. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea)

Wito huo umetolewa hivi karibuni na wafanyabiashara hao wakizungumza na MwanaHALISI, Online wilayani Kilwa, Mkoa wa Lindi.

Kiongozi wa wafanyabishara katika Bandari ya Jimbiza, Said Sheha, amedai amri ya wao kuondolewa ni kinyume cha sheria kwa kuwa sehemu ya eneo hilo liko kisheria kwa ajili ya shughuli za kijamii, kwani liko ndani ya mita 60 kutoka ufukwe wa bahari.

Sheha anadai, sehemu ya eneo hilo lina makaburi zaidi ya 200 ya ndugu zao waliozikwa miaka mingi iliyopita, huku akihoji hatma ya makaburi hayo kwa kuwa mwekezaji ameshaanza kujenga uzio kwa ajili ya maandalizi ya ujenzi wa hoteli yake.

“Hili eneo wazee wamerithi kutoka kwa wazazi wao na sehemu ya eneo hili lilitengwa kwa ajili ya shughuli za mazishi… cha kushangaza tunaambiwa tutoke tukatafute eneo lingine sasa hatma ya makaburi ya ndugu zetu itakuwaje? Na kwa nini muwekezaji auziwe makaburi?” amesema Sheha.

“Mnamo Mei mkuu wa wilaya alikuja akatuambia tuondoke na kwamba Rais amesema maeneo yote apewe muwekezaji, tukaenda kwa mwenyekiti wa CCM wilaya ya Kilwa, Said Ally, tukampa kilio chetu akatuchukua mpaka kwa mkuu wa wilaya tukazungumza naye akatuahidi atakuja na wataalamu wake kupima eneo la mita 60, ili tukabidhiwe lakini hadi leo hajafanya cha kushangaza wiki mbili zilizopita tunaona muwekezaji anajenga ukuta,” amedai Sheha.

Naye Athuman Mwichande, amedai viwanja alivyopewa mzungu kuwekeza ni namba 106 na 107, ambapo kiwanja namba 106 ndicho kimeingia kwenye sehemu kubwa ya eneo ambalo wananchi wanafanya shughuli zao na liko ndani ya mita 60 kutoka ufukwe wa bahari, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.

Mfanyabiashara wa samaki katika bandari hiyo, Mariam Mwichande, amemuangukia Rais Samia akimtaka aingilie kati ili wasiondolewe kwa madai kuwa hawana eneo lingine la kwenda kufanya biashara ili wapate ridhiki.

“Tunatoa kilio chetu kwa sababu mkuu wa wilaya katuambia tuhame kabisa, vitu vivunjwe apewe mwekezaji. Sisi tunakuomba Rais Samia utusaidie sababu tunalipa ushuru, tunapata fedha za kusomesha watoto wetu. Wewe mwanamke mwenzetu tusaidie.

Mfanyabiashara mwingine ambaye hakutaka kutaja jina, ameiomba Serikali imtafutie eneo lingine mwekezaji kwa ajili ya kuwekeza, ili wao wabaki katika eneo hilo kwa kuwa sehemu yake liko ndani ya mita 60 kutoka ufukwe wa bahari, lakini pia kuna makaburi ya ndugu zao.

“Najua serikali ina uwezo wa kuangalia wapi kuna wananchi kwa wingi wanafanya shughuli zao wawaache na inaweza kumtafutia mwekezaji eneo lingine akawekeza,” amesema.

Chanzo cha mgogoro huo kinadaiwa kuwa, aliyekuwa mmiliki wake Selemani Mwinyi, alidhulumiwa na Shaweji Mjaka, miaka 30 iliyopita na kwamba 2003 aliamua kuliuza kwa wawekezaji.

Akifafanua sakata hilo, Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Christopher Ngubiagai, amedai mwekezaji huyo anamiliki eneo hilo kihalali na kwamba alinunua kutoka kwa Majaka, baada ya Halmashauri ya Wilaya y Kilwa, kulipima kisha kuuza kwa wananchi.

Amedai, muwekezaji huyo tangu aliponunua analipia kodi ya ardhi, lakini pia hati ya umiliki iko katika Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).

Kuhusu madai ya viwanja hivyo kuingia ndani ya mita 60 kutoka ufukwe wa bahari kinyume cha sheria, pamoja na kuwa na makaburi, Ngubiagai amejibu akidai “sio kweli eneo halijaingia ndani ya mita 60 na wala hajajenga ndani ya mita 60. Wala makaburi hayako ndani ya eneo alilojenga.”

Akielezea chanzo cha mgogoro huo, Ngubiagai, amedai ulianza baada ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, kuandika barua kwenda kwa katibu tawala mkoa wa Lindi, ikitaka kampuni ya Kilwa Yark Club, kupewa viwanja vyake kwa ajili ya kuanza uwekezaji.

Ambapo yeye alichukua jukumu la kutekeleza agizo hilo kwa kuwataka wafanyabiashara kuondoka kwenye eneo la mwekezaji.

Ngubiagai amedai baada ya kutoa agizo hilo, aliwataka wakafanye  shughuli zao ndani ya eneo la mita 60 kutoka ufukwe wa bahari, ambalo wanaruhusiwa kwa mujibu wa sheria.

“Hata tulivyokuwa na mkutano nao tulikubaliana hizi prot mbili (106 na 107), wamuachie mwekezaji sababu hata mimi sina mamlaka ya kufuta hati alizopewa. Lakini hizi mita 60 ndugu zangu, wapiga kura wa Rais Samia, zitumieni kwa shughuli za kiuchumi. Nashindw akuelewa kwa nini wanasiasa wameingia kulikoroga suala hili,” amesema Ngubiagai.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari Mchanganyiko

NMB yang’ara maonesho OSHA

Spread the loveBenki ya NMB imebeba tuzo ya kampuni bora kwenye sekta...

BiasharaHabari Mchanganyiko

NBC yashiriki maadhimisho Mei Mosi Arusha

Spread the loveBenki ya Taifa ya Biashara (NBC) imeungana na maelfu ya...

Biashara

Promosheni ya bil 1 kutoka Meridianbet kasino, cheza na ushinde zawadi kubwa

Spread the love  INGIA katika ulimwengu wa zawadi za kushangaza: Jishindie sehemu...

BiasharaHabari Mchanganyiko

Equity Bank yaendelea kusotea mabilioni ya fedha mahakama rufani

Spread the loveBENKI za Equity ya Tanzania na Kenya, zimeendelea kupambana mahakamani...

error: Content is protected !!