Monday , 27 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Wabunge wamburuza Spika Ndugai kortini
Habari za SiasaTangulizi

Wabunge wamburuza Spika Ndugai kortini

Spread the love

SAKATA kati ya Spika wa Bunge, Job Ndugai na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad, limeanza kuchukua sura mpya, kufuatia wabunge wake wanne, kwenda mahakamani, kulishitaki Bunge. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Wabunge walioamua kwenda mahakamani, ni Zitto Kabwe (Kigoma Mjini); Saed Kubenea (Ubungo); Salome Makamba (Viti Maalum); Hamidu Bobali (Mchinga) na Anthony Komu (Moshi Vijijini).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Zitto kwa waandishi wa habari, leo Jumapili, tarehe 13 Januari, wabunge hao wameamua kufungua kesi ya Kikatiba Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, kuomba zuio la utekelezaji wa amri ya Spika.

Hatua ya wabunge hao, imekuja wiki moja, tangu Spika Ndugai, kuagiza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Kinga, Maadili na Madaraka, kumuita Prof. Assad, ili kuhojiwa juu ya madai ya kuliita “Bunge dhaifu.”

Akizungumza na waandishi wa habari, ofisini kwake mjini Dodoma, Jumatatu iliyopita, Spika Ndugai alimtaka Prof. Assad, kufika kwa hiari yake, mbele ya Kamati ya Bunge, tarehe 21 Januari mwaka huu.

Alisema, Prof. Assad anatakiwa kufika mbele ya kamati hiyo, ili kuhojiwa kwenye kile alichokiita, madai ya “kulidhalilisha Bunge.”

Ndugai alidai kuwa Prof. Assad, akiwa nchini Marekani, ambako alihudhuria mkutano wa wakaguzi wa mahesabu ulimwenguni, alinukuliwa akisema, Bunge limekuwa dhaifu na hivyo limeshindwa kutimiza wajibu wake.”

Akaongeza, “iwapo Prof. Assad hatafika mbele ya kamati hiyo kwa hiari, nitaelekeza akamatwe na kuletwa bungeni kwa pingu.”

Hata hivyo, tayari Prof. Asaad, “amemjibu spika Ndugai kwa kusema, “anapaswa kuwa mfano bora wa kuheshimu, kuilinda na kuitetea Katiba ya Nchi.”

Amesema, “sitaki kuwa miongoni mwa waivunjao katiba…Ibara ya 18 (a) inampa kila mtu uhuru wa kutoa maoni. Nayo Ibara ya 26 (1), ya Katiba ya Jamhuri, inaelezea wajibu wa kila mtu kufuata na kutii katiba ya nchi.

Akizungumzia shauri hilo, Zitto alisema, yeye na wenzake wameamua kwenda mahakamani kuomba tafsiri ya kisheria juu ya mipaka ya Kinga ya CAG pamoja na mamlaka ya Spika wa Bunge kuweza kumshtaki mwananchi bila kuathiri Uhuru wa maoni kikatiba.

Amesema, “tunapenda ifahamike kwa umma kuwa sisi hatumtetei Prof. Mussa Juma Assad, bali tunatetea heshima na uhuru wa ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (NAOT). Tunaamini kuwa hatua hii aliyochukua Spika Ndugai, ikiachwa itaweka msingi (Precedence) mbaya wa CAG kuingiliwa uhuru wake na taasisi mbalimbali kinyume na Katiba.”

Anaongeza, “ikumbukwe kuwa Bunge la Tanzania ni mdau na mteja wa CAG, kwani Hesabu za Bunge hukaguliwa na CAG. Lakini pia hesabu za taifa zima anazokagua CAG, hufikishwa bungeni kama mamlaka ya usimamizi wa serikali ili kuchukua hatua mbalimbali.

“Iwapo tutaruhusu ofisi ya CAG kutomaswa tomaswa na wakaguliwa wake, tunaweka hatarini hadhi, sifa na heshima ya mkaguzi m mbele ya umma.”

Kwa mujibu wa Zitto, wabunge hao wanne, wamemuagiza wakili mashuhuri wa kujitegemea na ambaye ni rais wa chama cha wanasheria Tanganyika (TLS), Fatma Karume, kufungua shauri hilo mahakamani mara moja.

MwanaHALISI Online iliwatafuta wabunge wengine watatu waliotajwa na Zitto kuwa wanakwenda mahakamani kufungua shauri hilo – Kubenea, Makamba na Bobale – ambao wote wamethibitisha jambo hilo.

Akizungumzia hatua hiyo, Makamba amesema, “kama alivyoeleza mheshimiwa Zitto, ni kwamba mimi na wenzangu, tumeamua kwenda mahakamani kuomba mahakama itoe tafsiri ya Kinga ya CAG iliyopo kikatiba; tafsiri ya Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge Katika kushtaki watu wanaosemekana kudharau Bunge.”

Anaongeza, “tunakwenda kuhoji mamlaka ya Spika wa Bunge la Jamhuri kuweza kumuita mtu yeyote kuhojiwa kwenye Kamati ya Maadili ya Bunge bila Azimio la Bunge zima.

Aidha, Makamba anasema, “tunakwenda kuiomba mahakama imzuie Prof. Assad na mdhibiti mkuu wa hesabu za serikali, kuitikia wito wa spika.”

Jingine ambalo wabunge hao wanakwenda kuliomba mahakamani, ni kumkataza spika kutekeleza wito wake kwa CAG, kwa kuwa ni kinyume na Katiba.

Kesi hiyo ambayo imepangwa kusajiliwa kwa hati ya dharura, inatarajiwa kufunguliwa kesho Jumatatu.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari MchanganyikoHabari za Siasa

Wazanzibar watarajia makubwa kutoka NMB Pesa Akaunti

Spread the loveWateja wapya wa Benki ya NMB wa Zanzibar wanatarajia neema...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Kinana aungana na Tale kugawa mitungi ya gesi 800

Spread the loveMAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Abdulrahman...

Habari za SiasaTangulizi

Makonda amjibu Mwenyekiti UWT, “wananipa nguvu ya kuwapiga spana”

Spread the loveMKUU wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amemshukia Mwenyekiti wa...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Madeni ya bilioni 219 yalipwa, wadai wengine waitwa

Spread the loveSERIKALI imesema kuanzia Mei mwaka 2021 hadi sasa imelipa madai...

error: Content is protected !!