December 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Zitto aibua madai mapya CAG & Ndugai

Aliyekuwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad

Spread the love

ZITTO Zuberi Kabwe, mbunge wa Kigoma Mjini na kiongozi mkuu wa chama cha ACT-Wazalendo, ameamua sasa “kulipasua jipu.” Anandika Faki Sosi … (endelea).

Anasema, kinachomsababishia misukosuko Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad, ni msimamo wake wa kukataa kuisafisha serikali.

“Ripoti ya CAG ya upotevu wa 1.5 trilioni ndio sababu ya kuundiwa zengwe kwa Prof. Assad. Wanataka kumuondoa kwenye nafasi yake kwa hoja kuwa hana mahusiano mazuri na taasisi anazoziongoza,” anaeleza.

Zitto alitoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari, makao makuu ya chama chake, Kijitonyama, jijini Dar es Salaam.

Anasema, “kikatiba CAG hawezi kuondolewa, lakini watasema kuwa hana mahusianao mazuri na Spika wa Bunge. Wanataka kumsimamisha kwa hoja ya kumchunguza, ili aje kaimu wake ambaye ataiondoa ripoti ya upotevu wa Sh. 1.5 trilioni.”

Kwa mujibu wa mbunge huyo, mpaka sasa, ofisi ya Spika wa Bunge, haijaipeleka ripoti maalum ya ukaguzi ya Sh. 1.5 trilioni kwa Kamati za Bunge za PAC na PAC.

Zitto amewahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mahesabu ya Mashirika ya Umma (POAC) na baadaye akachaguliwa kuwa Mahesabu ya Fedha za Serikali (PAC).

Amesema kuwa yeye ni mbunge wa muda mrefu bungeni mwenye miaka 13 anajua kuwa huo ni mchezo wa kuzuia wananchi wasijue jinsi utafutaji wa Sh. 1.5 trilioni ulivyofanyika; kutokana na uimara wa Prof. Assad, ndio maana wanamtengenezea zengwe ili ajiuzulu.

“Prof. Assad ni mtu madhubuti sana. Hageuzwi geuzwi. Kuna matumizi mabaya ya fedha za umma ambayo yamefanya kinyume cha Katiba na kinyume cha Sheria.

“Hayakuwa kwenye bajeti…kuna miradi mingi iliyotekelezwa bila kufuata sheria za fedha za nchi yetu. Ofisi ya CAG imeyaona haya, serikali haijaweza kutoa majibu,” anaeleza.

Anasema, “unamtoaje CAG kinyemela? Haiwezekani. Ndio maana wanatengeneza mgogoro feki kupitia kwa spika.”

Akiongea kwa kujiamini, Zitto alidai kuwa lengo la mkakati huo, ni “kutengeneza zengwe litakalomlazimisha CAG kukaa pembeni kwa muda, ili kupitisha ripoti ya Sh.1.5 trilioni.”

Anasema, “mimi na najua kwamba Ndugai na CAG walizungumza na waliombana radhi na yaliisha. Lakini kuna mtu alimtikisa Ndugai kuwa yasiishe. Tunajua sababu. Ni hizi fedha (Sh. 1.5 trilioni). Hicho ndio chanzo kikuu cha mgogoro huu wa sasa.”

error: Content is protected !!