Thursday , 2 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Wabunge waikalia kooni TAKUKURU Bungeni
Habari za Siasa

Wabunge waikalia kooni TAKUKURU Bungeni

Mwita Waitara
Spread the love

 

BAADHI ya wabunge wamelia na changamoto za utendaji wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), wakidai imekuwa chanzo cha vitendo vya ubadhirifu wa fedha za umma kwenye miradi ya maendeleo kuongezeka. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Malalamiko hayo yameibuliwa leo tarehe 19 Aprili 2024, bungeni jijini Dodoma, wakati wabunge wakichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa mwaka wa fedha wa 2024/25, iliyowasilishwa na waziri wake, George Simbachawene.

Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina, amehoji kwa nini madudu yanayoibuliwa katika ripoti za ukaguzi za Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), hayaonekani katika ripoti za taasisi nyingine za uchunguzi, ikiwemo TAKUKURU.

“Kutowiana kwa taarifa za uchunguzi na ukaguzi ni changamoto, wakaguzi wanakagua na kubaini kila dalili za wizi lakini ukienda TAKUKURU hakuna taarifa, hawasemi kama ni wizi au nini kimetokea. Mwaka jana tuliona ufisadi mkubwa katika ujenzi wa Bwawa la Kufua Umeme la Mwalimu Nyerere, IPTL, ujenzi wa reli ya kisasa na kadhalika, wahusika wote wanajulikana lakini ukienda TAKUKURU hakuna taarifa zao,” amesema Mpina.

Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina

Mbunge wa Sikonge (CCM), Joseph Kakunda, amedai baadhi ya viongozi wa TAKUKURU ngazi ya mikoa na wilaya, wanashindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo kiasi cha kupelekea taasisi nyingine kuibua ufisadi wakati wao wamepewa dhamana hiyo.

“TAKUKURU tuliwapa meno makubwa sana kupitia sheria, lakini kadri siku zinavyokwenda wale watu wetu kama vile wanapotea anaonekana mkurugenzi mkuu, lakini mkuu wa TAKUKURU wilaya na mkoa kama vile wanapotea. Anakuja kuonekana waziri mkuu anaibua mambo, anakuja CAG na mbio za mwenge zinaibua mambo lakini wao wapo. Inatakiwa waziri aangalie kama wanahitaji msaada wasaidiwe,” amesema Kakunda.

Katika hatua nyingine, Kakunda ameitaka Sekretarieti ya Maadili ya Utumishi wa Umma, itekeleze majukumu yake ya kusimamia maadili ya watumishi kuanzia ngazi ya juu hadi chini, badala ya kujikita zaidi katika zoezi la kujaza fomu za maadili za vigogo wa serikalini.

Kwa upande wake Mbunge wa Tarime Vijijini (CCM), Mwita Waitara, amesema “TAKUKURU imepewa jukumu kubwa kwanza la kuzuia rushwa lakini pia kuchunguza na kuthibitisha hatimaye wale watuhumiwa kuchukuliwa hatua za kisheria. Lakini kumekuwa na uchunguzi usioisha katika maeneo mbalimbali, yaani ikitokea kuna mradi unashukiwa kwa rushwa, wanaingilia kati uchunguzi hauishi miradi inasimama.”

“Naomba waziri eneo hili lifanyiwe kazi ili kama kuna tatizo mahali uchunguzi uishe, wanaowajibishwa wawajibishwe ili miradi iendelee. TAKUKURU wanaweza kusaidia huu uchafu wa hali ya hewa kwa kazi za serikali katika kila ripoti ya CAG upungue,” amesema Waitara.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Serikali yaanza msako wanaotoa mikopo kausha damu

Spread the loveSERIKALI imeanza kufuatilia watu, vikundi na taasisi zinazotoa kinyume cha...

Habari za Siasa

Spika Tulia aibana Serikali mafao ya wastaafu Jumuiya ya Afrika Mashariki

Spread the loveSPIKA wa Bunge, Dk. Tulia Ackson ameitaka Serikali kufanya tathimini...

Habari za Siasa

Serikali yawapa maagizo Ma-RC udhibiti magonjwa yasiyoambukiza

Spread the loveWAKUU wa mikoa nchini wametakiwa kuandaa utaratibu wa kuwawezesha wananchi...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mavunde ataja malengo “Vision 2030”

Spread the loveWAZIRI wa Madini amesema dhana ya “Vision 2030” inakusudia kuiendeleza...

error: Content is protected !!