November 29, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Vijana watakiwa kuwa mstari wa mbele kupinga sheria zinazominya uhuru wa kujieleza

Wakili Jebra Kambole

Spread the love

UHURU wa Wananchi kujieleza katika masuala mbalimbali sambamba  na kupewa taarifa juu ya masuala muhimu  yanayolihusu Taifa,  yanatajwa kuwa miongoni mwa masuala muhimu  kutekelezwa ndani ya Taifa lolote linaloheshimu na kulinda misingi ya haki za binadamu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Hayo yamebainishwa na Wakili Jebra Kambole  Septemba 24, 2022 wakati  wa Mdahalo ulioandaliwa na Jukwaa la vijana la ‘Reach Out Tanzania’ uliofanyika Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam na kuwashirikisha vijana kutoka makundi mbalimbali wakiwemo wanasiasa pamoja na waandishi wa habari wenye lengo la kujengeana uelewa juu ya masuala yahusuyo demokrasia.

Akizungumza  katika mdahalo huo, Jebra amesema Taifa lolote linaloheshimu na kusimamia misingi ya sheria ni lazima lijenge misingi ya wananchi wake kujieleza lakini pia kupewa taarifa za kitaifa zinazowahusu zikiwemo  kuhusu njaa, magonjwa na  zinginezo kwa kuwa ni haki yao kwa mujibu wa katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania inayompa haki kila mwananchi .

“Uhuru wa kijieleza na watu kupata taarifa ni suala muhimu katika Taifa lolote lile lenye uhuru wa kidemokrasia ni kawaida sana kuambiwa kuwa hakuna uhuru usio na mipaka, lakini huo mpaka lazima uwe na sheria na siyo tamko la mtu,” amesema Kambole.

Alisema sheria nyingi ambazo zimewekwa nchini hazipambanui moja kwa moja  ni makosa yapi yapo ndani ya vifungu hivyo ili kumfanya yule anayedaiwa kuivunja atambue kosa lake moja kwa moja lakini pia sheria hizo zinapaswa kuwa na adhabu zake zinazoendana na kosa husika.

Alitolea mfano sheria katika vyombo za habari nchini ambapo amesema nyingi zina mapungufu na kusababisha  matokeo yake waandishi na vyombo vya habari kujikuta wakiangukia katika adhabu ambazo msingi wake umetokana na mapungufu yaliyopo ndani ya sheria hizo.

 Alisema ni vyema Serikali na Bunge likaona umuhimu wa kuzifanyia marekebisho sheria zote zinazoonyesha kuwa na ‘ukakasi’ wa kutotafsiri vyema kilichozungumzwa ndani yake kwa ajili ya manufaa ya kila  mwananchi na hata kizazi kijacho.

Aidha alisema wanasiasa ni miongoni mwa watu wenye nafasi kubwa ya kuleta mabadiliko nchini kwa Taifa lolote ikiwemo Tanzania kutokana  nguvu pamoja na ushawishi walionao katika masuala mbalimbali yakiwemo ya kijamii, kiuchumi  kwani wao  ndiyo chachu katika maendeleo ya mataifa yao.

Katika mdahalo huo ulioongozwa na mada inayosema ‘Wajibu wa Raia kupata haki yake Kidemokrasia’ Kambole alisema hata sera pamoja na sheria mbalimbali zinazoanzishwa na kutumika nchini baadhi zimetungwa na wanasiasa hao kisha kupitishwa na Bunge hatua inayoonyesha wazi nguvu ya kundi hilo katika masuala mengi yanayohusu nchi.

Kwa upande wake  Mwenyekiti wa Ngome ya vijana wa chama cha ACT- Wazalendo Abdul Nondo amesema viongozi wanapochaguliwa wana wajibu wa kutekeleza Sera na sheria ambazo zitakuwa na manufaa kwa wananchi na nchi kwa ujumla.

“Umechaguliwa kuwa Mbunge, kuwa Diwani wajibu wako ni kwenda bungeni, kwenda halmashauri kuhakikisha kwamba unasimama kikamilifu kuwakilisha waliokutuma ili kuhakikisha sheria na Sera mbalimbali zinapitishwa kuwa na manufaa ya wananchi”

Aidha Nondo ameongeza kuwa vyama vya siasa nchini vina wajibu wa kuimairisha demokrasia ili hata vinapokuja kushika madaraka iwe ni sababu kuendelea kuimarika kwa demokrasia nchini.

“Kwahiyo vyama vya siasa ili kuweza kutengeneza utamaduni wa kuheshimu misingi ya kidemokrasia na Uhuru wa watu kutoa maoni ni lazima vyama vyenyewe vijiimrishe kwa kuwa na demokrasia imara,” ameongeza Nondo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kanda ya Kati Chadema Aisha Luja alisema katiba mpya ndiyo mwarobaini pekee wa changamoto zinazojitokeza nchini hivyo kuna haja ya kuhakikisha inapatiakana mapema iwezekanavyo kuleta ufumbuzi.

Alisema mapungufu yaliyopo ndani ya katiba hiyo ya Mwaka 1977, ndiyo hasa inayopelekea hadi leo watu wanalaumu na kulalamika kila wakati huku jukumu la kudai katiba hiyo wakiliacha mikononi kwa wanasiasa pekee.

“Kama katiba inayodaiwa hapa ni ya watanzania, kila mtanzania ana wajibu wa kuhakikisha anasimama na kuidai, lakini vyama vya siasa sote bila kujali ukubwa au udogo wetu  tunapaswa kudai katiba hiyo kwa sababu sote tunawawakilisha wananchi.

Naye Mkurugenzi wa Jukwaa la Reach Out Tanzania, Kumbusho Dawson amewashukuru wadau waliojitokeza katika mdahalo huo wa Siku mbili huku  akiongeza kuwa  mapendekezo yaliyotolewa na wadau katika mdahalo huo watahakikisha wanayafanyia kazi pasi na kukiuka misingi ya katiba ya nchi.

error: Content is protected !!