RAIS wa Kenya, Dk. William Ruto jana tarehe 27 Septemba, 2022 amemteua Japhet Koome kuwa Inspekta Jenerali mpya wa Jeshi la polisi nchini humo kuchukua nafasi ya Hilary Mutyambai. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Kwa mujibu wa Rais Ruto, hatua hiyo imetokana na ombi la kujiuzulu la Hilary Mutyambai kutokana na kile alichosema ni matatizo ya kiafya.
Baada ya uteuzi huo jina laKoome litapelekwa bungeni ili kupigwa kura na kuidhinishwa.
Mutyambai ambaye alikuwa amebakisha miezi sita kustaafu, hajaripoti kazini tangu mwezi Agosti kwa kile kilichosemekana kuwa matatizo ya kiafya.
Wadhifa wake ulikuwa ukishikiliwa na Noor Gabow, ambaye alikuwa akipigiwa upatu kuteuliwa kuchukua mahali pa Mutyambai.
Rais Ruto pia alitangaza kujiuzulu kwa Mkurugenzi wa Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI), George Kinoti, na kusema Idara ya Huduma za Polisi itamteua mrithi wake karibuni.
Wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa tarehe 9 Agosti, 2022 mrengo wa Kenya Kwanza unaoongozwa na Rais Ruto ulimlaumu Mutyambai kwa kile ulichosema ni kukubali polisi kutumiwa kisiasa.
Kinoti naye alilaumiwa kwa madai ya kutumiwa na serikali ya Rais Uhuru Kenyatta kuwahangaisha waliokuwa wakimuunga mkono.
Leave a comment