Wednesday , 1 May 2024
Home Habari Mchanganyiko TUICO wauburuza mahakamani uongozi Yacht Club madai udhalilishaji
Habari Mchanganyiko

TUICO wauburuza mahakamani uongozi Yacht Club madai udhalilishaji

Wakili Raymond Mweri
Spread the love

CHAMA cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO) tawi la Dar es Salaam Yacht Club kimewafungulia shauri la madai ya fidia menejimenti ya kampuni hiyo katika Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam kwa madai ya udhalilishaji. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana tarehe 25 Aprili, 2022 kwa niaba ya TUICO, Wakili Raymond Mweri alisema katika shauri hilo la madai, wanataka kulipwa fidia ya Sh milioni 500 kutokana na athari walizozipata.

Dar es Salaam Yacht Club ni kampuni inayojihusisha na michezo ya baharini

Alisema kesi hiyo ambayo itaanza kuunguruma muda wowote ndani ya wiki mbili, imetokana na kauli zilizotolewa na meneja wa kampuni.

Akifafanua kwa kina msingi wa shauri hilo, Wakili Mweri alisema mwaka 2018 uliibuka mgogoro baina ya menejimenti ya Dar es Salaam Yacht Club na wafanyakazi wao kupitia Tuico.

“Msingi wa mgogoro huo wafanyakazi walikuwa wanaituhumu na kuilalamikia menejimenti ya Dar es Salaam Yacht Club kwa tuhuma mbalimbali ikiwamo matumizi mabaya ya madaraka pamoja na kutumia mbinu ambazo si njema zinazodhihirisha nia ovu ya kuwashawishi baadhi ya wafanyakazi ambao ni walikuwa ni wanachama wa TUICO kujitoa kwenye chama hicho.

“Mgogoro huo uliendelea kufukuta hadi tarehe 9 Oktoba 2021, kupitia vyombo vya habari vilimnukuu kiongozi wa Dar es Salaam Yacht Club akitamka kwamba wafanyakazi wake wamekuwa wakitumika vibaya na wahalifu,” alisema.

Alisema kauli hiyo iliwafanya TUICO tawi la Dar es Salaam Yacht Club kusikitishwa na tamko hilo.

Aliongeza kuwa kwa kutambua kwamba kwa mujibu wa sheria zilizopo nchini zipo zinazotambua na kutoa utaratibu wa namna ambavyo kosa la udhalilishaji linavyoweza kuchukuliwa hatua.

“Ndipo wakachukua hatua za kisheria ambapo tarehe 20 Disemba, 2021 walituma barua ya madai kwamba TUICO kwa kuamini kuwa wao ndio wanaotetea masilahi ya wafanyakazi husika, tamko la kuitwa wahalifu au tamko la Meneja wa kampuni hiyo kwa namna moja au nyingine liliwadhalilisha.

“Msingi wa barua ile ilikuwa kuwaeleza kwamba wamedhalilishwa na kuwapa muda Dar es Salaam Yacht Club kurekebisha kitendo hicho ambacho TUICO walikitafsiri kama kitendo kiovu.

“Pia waliwaelekeza waombe radhi kupitia vyombo vya habari ambavyo vilitumika kutoa tamko hilo na Dar es Salaam Yacht club wafidie Sh milioni 500 kwa athari walizopata kutokana na matamko hayo,” alisema.

Aidha, alisema tarehe 20 Januari, 2022, menejimenti ya Dar es Salaam Yacht Club walijibu barua hiyo na kupinga madai hayo ndipo TUICO wakaamua kuchukua taratibu za kufungua shauri rasmi kwa mujibu wa sheria zilizopo nchini.

“Tumezingatia sheria ya ‘The Media Services Defamation proceeding rules’ ambayo inaelekeza hatua za kufuatwa pindi taasisi au mtu anapokuwa amedhalilishwa kwa matamko ya kutamkwa mdomoni au ya maandishi.

“Machi mwaka huu tumeshafungua shauri ambalo kwa mujibu wa sheria na ndani ya siku saba tumeshawatumia hati ya madai Dar es Salaam Yacht Club na mahakama kuu tumempeleka nyaraka ya kiapo ikieleza utaratibu ambao umefuatwa katika kufungua hati ya madai ikiwa ni pamoja na anuani na wahusika waliohusika kupokea hiyo petition,” alisema.

Alisema kutokana na taratibu zinazoendelea, sasa wana wito ambao wataupeleka upande wa pili (Dar es Salaam Yacht Club) na kuwa tayari kusubiri kesi hiyo kuunguruma.

“Suala la hoja kwamba tamko lililotolewa na Meneja wa Dar es Salaam Yacht Club kama ni kosa kwa mujibu wa sheria au lah, hilo tunaiachia mahakama.

“Sasa wajibu wetu ni kuhakikisha tunaidhibitisha Mahakama kuwa haya maneno yaliyotamkwa na menejimenti ya Dar es Salaam Yacht kwamba TUICO wamedhalilishwa na wanastahili fidia,” alisema.

Alisema wameamua kuchukua hatua hiyo hasa ikizingatiwa TUICO wana wanachama nchi nzima, kwa hiyo kimsingi kudhalilishwa ni sawa na kuwadhalilisha wanachama wote.

“Hivyo tunakwenda kutengeneza heshima kwa wanachama wa TUICO na hata watanzania kwa ujumla tunataka kuona wakinufaika na mwisho wa kesi hii,” alisema.

Aidha, Mwandishi wetu aliutafuta uongozi wa Dar es Salaam Yacht kupitia Afisa Rasilimali watu, Stella Kimaro ambaye hakupokea simu na hata alipotumiwa ujumbe mfupi kuhusu madai hayo hakujibu chochote.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

NEMC yatoa elimu matumizi sahihi ya zebaki kwa wachimbaji

Spread the loveBARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC)...

BiasharaHabari Mchanganyiko

Oryx gesi yagawa mitungi, majiko 100 kwa waandishi wa habari Dar

Spread the loveKAMPUNI ya Oryx Gesi Tanzania imegawa mitungi 100 ya gesi...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mavunde ataja malengo “Vision 2030”

Spread the loveWAZIRI wa Madini amesema dhana ya “Vision 2030” inakusudia kuiendeleza...

Habari MchanganyikoMichezo

Wanamichezo Mei Mosi wachangia wahitaji vitu vya mil. 11.5

Spread the loveWanamichezo wanaoshiriki Michezo ya Mei Mosi Taifa 2024 jijini Arusha...

error: Content is protected !!