Spread the love

BENKI ya NMB nchini Tanzania, imeahidi kuendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha wakazi wa Mkoa wa Geita wanazidi kupata huduma bora hasa katika sekta ya elimu na Afya. Anaripoti Mwandishi Wetu… (endelea).

Hayo yalisemwa na meneja wa NMB Kanda ya Ziwa, Baraka Ladislaus wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya msaada wa vitanda, magodoro na mashuka katika kituo cha afya Katoro pamoja na kutoa madawati 200, meza 50 na viti 50 kwa shule za msingi na sekondari katika mkoa wa Geita.

“Jumla ya msaada tuliotoa leo ni vitanda 10,magodoro 10, mashuka 30 kwa kituo cha afya Katoro, meza 50 na viti 50 kwa shule ya sekondari Magenge, Madawati 50 kwa shule ya msingi Msufini na shule ya msingi Bahari madawati 50, Madawati 50 kwa shule ya msingi Mtakuja na madawati 50 kwa shule ya msingi mchongamani na vifaa vyote vya vinathamani ya shilingi milioni 30,” alisema Ladislaus.

Aidha, akimkabidhi mkuu wa mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule alimuhakikishia benki hiyo itaendelea kuchangia katika sekta hizi mbili kwani sera ya benki imelekeza katika kuchangia maendeleo ya sekta hizo na kusaidia yanapotokea majanga.

“Benki ya NMB inatoa shukran za dhati hasa kwa viongozi wa halmashauri ya wilaya ya Geita kwa ujumla pamoja na kamati mbali mbali kwa kuwa mstari wa mbele kuona sekta ya afya na elimu inapata vifaa stahiki na kuwa chachu ya kuifanya Katoro kuwa mji wenye mafanikio makubwa kielimu,” alisema meneja huyo wa NMB Kanda ya Ziwa.

“Pamoja na makubwa yanayofanya na Serikali, sisi kama wadau tunaowajibu wa kuunga mkono juhudi hizi za maendeleo kwa kusaidia jamii zetu kwani kupitia jamii hii ndio imefanya benki ya NMB kuwa hapa na kubwa kuliko benki yoyote hapa nchini ” alisema Ladislaus.

“Sisi kama benki ya NMB tulipopata maombi ya kuja kuchangia, tulifarijika na kuamua kuja mara moja kuchangia maendeleo ya sekta ya elimu na Afya haswa wilaya ya Geita na hususani katika kituo cha afya cha Katoro, shule ya sekondari Magenge na Shule za msingi Msufini, Bahari, Mtakuja na Mchongamani.

“Benki ya NMB itahakikisha jamii inayotuzunguka inafaidika kutokana na faidi tunayoipata.

“Kwa miaka kadhaa sasa,NMB tumekuwa tukisaidia miradi mbali mbali ya maendeleo kwa wananchi kwa kujikita zaidi kwa miradi ya elimu(Madawati,vifaa vya kuezeka),Afya(vitanda na magodoro pamoja na vifaa vya kusaidia matibabu),” alisema Ladislaus.

Alisema benki yao imekuwa mstari wa mbele kwa kuchangia huduma za kijamii kwa lengo la kurejesha sehemu ya faida yao kwa jamii. Huku kwa zaidi ya miaka saba mfululizo wametenga asilimia 1% ya faida kama sehemu ya uwajibikaji kwa jamii inayotuzunguka.

“Kwa mwaka 2022,NMB imetenga zaidi ya shilingi bilioni 2 kwajili ya kuchangia maendeleo ya jamii ikiwemo kusaidia sekta ya elimu na Afya. NMB tumefikia wilaya zote nchini kwa asilimia 100 na tunaendelea kuboresha huduma za kibenki kwa njia ya mitandao ili kuwafikishia huduma za kibenki wananchi wengi zaidi” alisema Ladislaus.

Kwa upande wake, Mkuu wa mkoa wa Geita,Rosemary Senyamule ameishukuru sana benki ya NMB kwa kuleta msaada katika kituo cha afya Katoro.

“Asante sana NMB mmendelea kuwa msaada mkubwa sana kwetu watu wa Katoro na Geita kwa ujumla nashukuru sana benki yenu imekuwa ikitoa msaada sana kwa Serikali yetu” alisema Senyamule.

Alisema benki ya NMB imekuwa kimbilio lao kila wanapokuwa wamepata changamoto. Aliahidi kuendeleza ushirikiano na benki ya NMB.

Naye mwalimu mkuu wa shule ya msingi Msufini, Anita Mahalu aliishukuru sana benki ya NMB kwa kuleta madawati shuleni kwao.

“Hakika benki ya NMB ni msaada mkubwa sana kwetu imetusaidia madawati hayo na shule yetu ina idadi ya wananfunzi 2377 wa darasa la awali mpaka shule ya msingi” alisema Mahalu. Alisema kwa sasa shule yao inakabiliwa na uhaba wa madawati 212.

Naye Kaimu Mganga mfawidhi wa kituo cha afya Katoro, Dk Rhoda Haule aliishukuru sana benki ya NMB kwa kuweza kuwasaidia vitanda na magodoro pamoja na mashuka.

Alisema licha ya msaada wa benki ya NMB bado wanakabiliwa na uhaba wa vitanda 45, mashuka 300 na mablangeti 300. Alisema kwa mwezi hospitalini kwao wanazaliwa watoto 800 na kwa mwezi wanalazwa wagonjwa 8000.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *