CHAMA cha ACT-Wazalendo, kimeeleza ‘kufurahishwa’ na wepesi uliofanya na Chama Cha Mapinduzi (CCM), ngazi ya urais Zanzibar. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).
Akizungumza na MwanaHALISI Online leo tarehe 13 Julai 2020 kuhusu uimara wa Dk. Hussein Mwinyi, mgombea wa CCM ngazi ya urais visiwani Zanzibar, Ado Shaibu ambaye ni Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo amesema, CCM imempeleka mgeni mwenyeji kugombea urais Zanzibar.
“Unajua Zanzibar moja ya mambo yanayowakera ni kuchaguliwa rais wasiyeishi naye. Wanasema wagombea wanaoishi nao huko kwao hawateuliwa, ila wanawateua wale waliopikwa Bara kwenda kuongoza Zanzibar.
“Kwa muktadha huo, Wazanzibari wengi hawako tayari kumchagua Dk. Mwinyi ambaye muda wote hapatikani Zanzibar, maisha yake yote ni huku Bara na kule anafuata kura tu,” amesema Ado.
Amesema, kwa muda mrefu Wazanzibari wamekosa mtu anayetokana na wao kwa maana ya kuishi maisha yake ndani ya visiwa hivyo.
Soma zaidi..
- Dk. Mwinyi: Nitakuja na staili ya Rais Magufuli
-
Urais Z’bar: CCM yampitisha Dk. Mwinyi
“Maalim Seif (Maalim Seif Sharif Hamad, mgombea urais kupitia ACT-Wazalendo) pamoja na uimara wake lakini amekuwa ni mwenyeji na mkazi wa Zanzibar.

“Wazanzibari wanaona huyu ndio mwenzao, wanakula naye vumbi wote, wanakutana naye mitaani, wanazungumza naye na wanakutana naye kwenye shughuli mbalimbali za kijamii, huyu ndio mwenzao,” amesema.
Tarehe 10 Julai 2020, Halmashauri Mkuu ya (CCM) ilimpitisha Dk. Mwinyi kwa asilimia 78 kuwa mgombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020.
Akitangaza matokeo hayo, Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai alisema, Dk. Mwinyi amepata kura 129 sawa na asilimia 78.65, Shamsi Vuai Nahidha kura 16 na Dk. Khalid Salum Muhamed kura 19.
Ado amesema, “Dk. Mwinyi ni mtu ambaye tunafahamu uwezo wake na udhaifu wake na kwetu sisi ni mgombea ambaye ni dhaifu zaidi, kwa hiyo hatubabaishi na tutapata ushindi mnono.”
Leave a comment