October 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Spika Tulia ataka kibano waajiri wasiopeleka michango mifuko hifadhi jamii

Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson

Spread the love

SPIKA wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, ameitaka Serikali iweke utaratibu mzuri wa kusimamia mifuko ya hifadhi ya jamii, ili iwabane waajiri wasiowasilisha michango ya fedha za wafanyakazi  katika mifuko ya hifadhi ya jamii. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Spika Tulia ametoa agizo hilo, leo Ijumaa, tarehe 23 Septemba 2022, bungeni jijini Dodoma, baada ya Mbunge Viti Maalum, Anastazia Wambura, kuhoji lini wastaafu ambao waajiri wao walikuwa hawatoi michango katika mifuko ya hifadhi ya jamii, watalipwa haki zao.

“Ofisi za wabunge zina malalamiko mengi sana ya wastaafu wa nchi hii na tukisema tutaliacha liendelee mtu atafuatilia mafao miaka miwili wanaambiwa michango yao haikuja. Kama ni kazi ya mfuko unajua mwajiri hajapeleka ni kazi yao mfuko umlipe huyu mafao yake, wao wakatafute pesa zilipo,” amesema Spika Tulia.

Spika Tulia amesema “sidhani kama wananchi wanatakiwa kuteseka baada ya kuwa wamelipa kwenye mifuko na muajiri ameshakata pesa. Serikali mtengeneze utaratibu mzuri wa kusimamia mifuko, izitafute hizo pesa iwalipe wastaafu.”

Baada ya Spika Tulia kutoa agizo hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu,-Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako, amesema Serikali inafanyia kazi suala hilo na kwamba baada ya miezi mitatu itapata suluhu ya tatizo hilo.

“Ni kweli kumekuwa na changamoto ya baadhi ya waajiri kutopeleka michango katika kifuko na hivyo kusababisha wastaafu ambao michango haijapelekwa ama kutopata mafao yao kwa wakati au kupata ambayo yana mapunjo. Serikali imeliona suala hilo na tunalifanyia kazi kupata ufumbuzi,” amesema Prof. Ndalichako na kuongeza:

“Kwa wale waajiri ambao malipo yameshakuwa na muda mrefu yapo ambayo yanafika miaka 10. Bado hawajaleta hizo fedha. Naomba nilihakikishie Bunge lako kwamba tayari Serikali inafanyia kazi na ninaahidi ndani ya miezi mitatu tutakuja na muafaka wa kutatua tatizo hili ambalo limekuwa kwa muda mrefu.”

Awali Naibu Waziri wa wizara hiyo, Patrobasi Katambi, akijibu swali la Wambura, amesema tayari Serikali imefungua akaunti ya mtandaoni ili kupata taarifa za waajiri wanaowasilisha michango, kitendo kitakachosaidia kuwabana wasiowasilisha.

“Serikali tumeshachukua utaratibu wa kufungua akaunti ya kimtandaoni ya moja kwa moja na kila mwanachama anapewa taarifa yake kupitia simu ya kiganjani. Kwa hiyo kama michango haendi kwa sasa tunawakamata. Tunaendelea na operesheni kali kuweza kufanya ukaguzi ili kuweza kuhakikisha takwa la kisheria linatimizwa,” amesema Katambi.

error: Content is protected !!