HATIMAYE Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia tarehe 23 Agosti, 2022 iwe siku ya mapumziko ili Watanzania wawepo majumbani na waweze kuwapokea makarani wa sensa na kutoa maelezo sahihi. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Uamuzi huo umekuja siku chache baada ya Kamisaa wa Sensa 2022, Anne Makinda kutoa ufafanuzi kwamba siku hiyo ya sensa tarehe 23 Agosti 23 mwaka huu, haitakuwa siku ya mapumziko badala yake kila mmoja ataendelea na shughuli za kimaendeleo .
Akizungumza katika Kongamano la viongozi wa dini pamoja na kuzindua tangazo la umuhimu wa ushiriki wa sense tarehe 3 Agosti, 2022, Makinda ambaye pia Spika mstaafu wa Bunge la Jamhuri alisema tarehe 23 itakuwa siku maalum ya kuhesabiwa lakini itaendelea taratibu za kuhesabu madodoso hadi tarehe 28 agost mwaka huu.
“Siku hii sio ya mapumziko kuna mtu nilimsikia akisema ni siku ya mapumziko hapana… kila mmoja ataendelea na shughuli zake ila atakuwa ameacha taarifa zake katika makazi ambayo alikuwa amelala siku ya zoezi la sensa” alisisitiza Makinda.
Hata hivyo, katika taarifa iliyowekwa kwenye akaunti za Ofisi ya Waziri Mkuu na msemaji mkuu wa serikali kwenye mtandao wa Twitter zimebainisha kuwa siku hiyo itakuwa ni ya mapumziko.
“Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Alhamisi amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia tarehe 23 Agosti 2022 iwe siku ya mapumziko ili Watanzania wawepo majumbani na waweze kuwapokea makarani wa sensa na kutoa maelezo sahihi”.
Leave a comment