Friday , 19 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Ujenzi BRT II wafikia asilimia 66.6
Habari Mchanganyiko

Ujenzi BRT II wafikia asilimia 66.6

Spread the love

WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amesema ujenzi wa mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT II), Awamu ya Pili kutoka Mbagala hadi Gerezani umefikia asilimia 66.6 na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Februari, 2023. Anaripoti Urumasalu Kisung’uda… (endelea).

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, akikagua hatua za ujenzi wa mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT II), Awamu ya Pili unaoanzia eneo la Mbagala hadi Gerezani ambao umefikia asilimia 66.6 na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Februari, 2023.

Prof. Mbarawa amesema hayo leo tarehe 18 Agosti, 2022 jijini Dar es Salaam baada ya kukagua ujenzi wa mradi huo ambapo amefafanua kuwa kazi zinaenda vizuri huku ikitarajiwa kuwa mradi huo kukamilika kwa muda uliopangwa ili uweze kupunguza msongamano wa magari na kurahisisha usafiri.

“Nimefurahi kazi inaenda vizuri ila bado nitakuwa nikija hapa kukagua mradi huu mara kwa mara ili kuhakikisha mkandarasi anamaliza kwa wakati na viwango kwa sababu mradi huu ni muhimu sana katika kurahisisha usafiri na kupunguza msongamano”, amesisitiza Prof. Mbarawa.

Aidha, Prof. Mbarawa amemtaka mkandarasi wa mradi huo kuhakikisha anakamilisha upande wa pili wa barabara za juu (flyover) ya Chang’ombe na Kurasini ifikapo mwezi Oktoba ili kuruhusu magari kupita juu huku kazi nyingine zilizobakia zikiendelea.

Amemtaka pia kukamilisha ujenzi wa daraja lenye urefu wa mita 80 eneo la BP ifikapo mwezi Desemba 2022 na madaraja mengine kukamilishwa mwezi Januari, 2023 ili kupunguza changamoto ya msongamano wa magari katika maeneo hayo.

Pamoja na hayo amewataka wananchi waliopo karibu na mradi huo kutoa ushirikiano kwa mkandarasi ili mradi huo umalizike mapema iwezekanavyo.

Kwa upande wake, Msimamizi wa mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT II), Mhandisi Frank Mbilinyi, amesema kuwa wanatarajia Daraja lililopo Bandarini kumalizika na magari kuanza kupita mwezi Oktoba mwishoni wakati madaraja mengine yameshakamilika kwa upande mmoja na magari yameruhusiwa kupita.

Mradi huu ni moja ya mkakati ya Serikali ya kupunguza msongamano katika jiji la Dar es Salaam ambapo unahusisha ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilometa 20.3, Daraja kubwa la Waenda kwa miguu eneo la Mbagala, vituo vya mabasi 27, karakana ya mabasi 1.

Pia utahusisha ujenzi wa vituo vikuu viwili vya mabasi (Terminals) eneo la Kariakoo na Mbagala, vituo vya mlisho (feeder station) 5 pamoja na barabara za juu (flyover) 2 eneo la Chang’ombe na Uhasibu ambazo zitagharimu takribani Shilingi bilioni 217.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

NEMC yaonya wanaojenga bila tathmini ya mazingira

Spread the loveBARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC),...

BiasharaHabari Mchanganyiko

NMB Pesa Akaunti yawavutia wakaguzi wa ndani Afrika

Spread the loveUbunifu wa bidhaa bora wa Benki ya NMB pamoja na...

Habari Mchanganyiko

Carbon First, Ruangwa wasaini makubaliano ya biashara ya hewa ukaa

Spread the love  KAMPUNI ya Carbon First Tanzania Limited na Halmashauri ya...

Habari Mchanganyiko

CBE yawakumbuka wenye mahitaji maalum Jangwani

Spread the loveCHUO cha Elimu ya Biashara (CBE), kimetoa msaada mbalimbali na...

error: Content is protected !!