November 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Shule yenye darasa moja tangu 2014

Spread the love

 

BWANAHERI Akili, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi, Namalombe iliyopo Nanyumbu mkoani Mtwara, ameiomba serikali kujenga madarasa mengine katika shule yake kwa kuwa, mpaka sasa ina darasa moja. Anaripoti Mwandishi Wetu, Nanyumbu … (endelea).

Amesema, darasa hilo lilijengwa mwaka 2014 lakini mpaka sasa, hakuna madarasa mengine hivyo kusababisha usumbufu kwa wanafunzi.

Ombi hilo liliongezwa mkazo na wanafunzi wa shule hiyo, wakati David Silinde, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), kufika katika shule hiyo wakati wa ziara yake, mkoani Mtwara.

Wanafunzi walimueleza Silinde kwamba, wanapata tabu kwa kufundishwa wakiwa chini ya mikorosho kutokana na kukosa madarasa kwa muda mrefu.

“Tunasomea chini ya mikorosho, tunapata tabu, tunaomba kujengewa madarasa,” wanafunzi hao walimueleza Silinde huku Mwalimu Akili akisitiza “tuna darasa moja tu tangu 2014.”

“Wanafunzi wa darasa la saba, darasa la kwanza na darasa awali wanalazimika kusoma chini ya mkorosho huku. Darasa la pili, tatu, nne, tano na sita wote wakisoma katika jengo la darasa moja lililopo, hivyo kufanya kiwango cha kufundisha kuwa kidogo huku wakitumia choo kimoja cha Nyasi wote (walimu na wanafunzi),” amesema Mwalimu Akili.

Silinde alifika katika shule hiyo, baada ya kupata taarifa kuwepo kwa shule yenye darasa moja.

Baada ya kushuhudia shule hiyo, Silinde alimwagiza Hamis Dambaya, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmshauri Wilaya ya Nanyumbu, kujenga madarasa manne haraka ndani ya miezi miwili.

Pia, amemuagiza kutenga bajeti ili kujenga nyumba za walimu, ofisi na madarasa mengine huku yeye (naibu waziri) akihaidi kujenga madarasa matatu kwa kutumia mfuko wa Tamisemi.

error: Content is protected !!