Monday , 26 February 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Shetani ameweka kambi Z’bar?
Makala & UchambuziTangulizi

Shetani ameweka kambi Z’bar?

Spread the love

NINAZIONA jitihada za nguvu na waziwazi za uongozi wa serikalini kuwasukumia wafanyakazi wa Shirika la Meli Zanzibar lawama na shutuma kuhusu kulala kwa meli ya Mv Mapinduzi II. Anaandika Jabir Idrissa…(endelea).

Tarehe 18 Aprili, anayeitwa Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, Dk. Sira Ubwa Mamboya alikwenda kuiona meli hii iliyotiwa nanga nje kidogo ya Bandari Kuu ya Malindi, mjini Zanzibar.

Akiwa ziarani, alitoa maelekezo ya msimamo wa Serikali kuhusu hatima ya Mv. Mapinduzi II na nyingine iliyopita chini ya shirika hilo; baada ya kuwa amepata maelezo ya menejimenti ya shirika.

Huyu Dk. Sira amekwenda ziarani na msimamo kwamba kwa namna yoyote ile, ni lazima meli hii ya Mv Mapinduzi II na nyingine zifanye kazi ya kutoa huduma kama zilivyokusudiwa.

Serikali kupitia maelekezo ya Dk. Sira inataka kuona Shirika la Meli linatumia maarifa yake yote na raslimali zilizo chini yake ili kuhakikisha meli zake zote zinatembea.

Anasema lengo kuu la kuundwa kwa shirika hilo ni kutoa huduma ya kusafirisha abiria na mizigo kati ya visiwa vya Unguja na Pemba na kwengineko; na kupata faida na sio hasara kwa serikali.

Isitoshe, waziri ametilia hima kwamba meli zifanye kazi ya kutoa huduma kwa kuwa amelalamikiwa hivi karibuni alipokuwa nchini Visiwa vya Comoro kuwa, wanapata shida ya usafiri sasa tangu kukosekana kwa huduma za Mv Mapinduzi II.

Kwamba, watu wa visiwa hivyo wamekuwa wakiitegemea meli hiyo kwa ajili ya usafiri wao pamoja na usafirishaji wa mazao ya vyakula mbalimbali kutoka Zanzibar.

Na kwamba wanaihitaji huduma ya Mv Mapinduzi II kipindi hiki cha kukaribia mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani wakitaka bidhaa mbalimbali za kilimo.

Akasema kwa kuwa, amejulishwa kwamba meli itapona kwa kuwa tatizo lake limeshajulikana na kwamba, mafundi tayari wapo kazini, hayuko tayari kuona lengo linashindikana kutekelezwa.

Na akasema kwamba, baada ya kazi ya matengenezo ya meli kwisha, Serikali “itawachunguza wafanyakazi wote wa meli hiyo… kuangalia upya vyeti vyao kama ni sahihi hasa kwa vile sababu kubwa ya kuharibika kwa meli hiyo ni suala la elimu ndogo ya wanyakazi ambao wawapo wasiokuwa na vyeti vya taaluma.”

Kwa mujibu wa taarifa ya kihabari niliyoisoma baada ya ziara, ikilengwa kujuza umma wa Wazanzibari kile hasa kilichotokea wakati wa ziara ya Dk. Sira, kwenye meli ya Mv Mapinduzi II, maelekezo yake yatekelezwe haraka na kwa ufanisi.

Maelekezo bila ya shaka yalitolewa naye baada ya kuwa ameikagua Mv Mapinduzi II. Na ni sawasawa kusema kuwa, maelekezo yalitolewa baada ya kutanguliwa na maelezo ya menejimenti ya shirika.

Alikuwa ni Mkurugenzi Muendeshaji wa Shirika la Meli Zanzibar, Salum Ahmada Vuai aliyetoboa siri hiyo ya kuwataja wafanyakazi kuwa, wana kasoro kitaaluma na ndio “sababu kubwa ya meli kuharibika.”

Naam! Kashfa ya kuharibika kwa meli ya Mv Mapinduzi II, iliyonunuliwa mwaka 2015, inatupiwa wafanyakazi wa meli yenyewe.

Hakuna ufafanuzi wa ni wafanyakazi wepi hasa wanaohusika na kuharibika meli hii? Hakuna, na wala hapakutolewa maelezo ya namna gani wameiharibu meli. Hakuna maelezo hayo.

Meli inayoelezewa hapa ni ile ambayo ununuzi wake ulifanywa na kilichoitwa Kamati ya kitaifa. Kamati hii iliongozwa na Omar Yussuf Mzee aliyekuwa Waziri wa Fedha na Uchumi wakati ule.

Chini ya Kamati ya Mzee, haijaelezwa hata mara moja kama hao wafanyakazi ambao sasa wanatupiwa tuhuma za kuwa “sababu kubwa” ya meli kuharibika walikuwemo katika msafara uliokwenda nchini Korea kupanga na kufuatilia mipango ya ununuzi wa meli.

Lakini kama hayo hayatoshi, hakuna maelezo ya kama kuna uchunguzi wowote uliofanywa hata kugundua kuwa hao wafanyakazi ndio walioiharibu meli.

Hakuna maelezo ya kwamba uharibifu wa meli unatokana na matumizi au uendeshaji wa meli baada ya kuzinduliwa na kuanza kazi ya kutoa huduma; au ni ufundi wake katika hatua ya upangalia na ufuatiliaji wa ununuzi.

Mzee aliyeongoza Kamati ya ununuzi wa Mv Mapinduzi II alipata kumhakikishia aliyekuwa Rais wa Zanzibar wakati huo, Dk. Ali Mohamed Shein kwamba, meli hiyo ni mpya tena “mpya kabisa.”

Meli hiyo ikatajwa kuwa ujenzi wake uliodumu kwa miezi 18 kufikia mapema Disemba 2015 ilipofika bandarini Zanzibar, uligharimu Dola za Marekani milioni 30.4 kiasi cha zaidi ya Sh. 40 bilioni za Tanzania.

Meli ilielezwa pia kuwa imejengewa mtandao imara wa kiufundi uliohusisha vifaa vya kisasa vya mawasiliano na vya huduma ya uokoaji kama vile boti ndogo na majaketi ya kupewa abiria wakati wa dharura.

Pamoja na yote hayo, Mv Mapinduzi II baada ya kufika haikuanza kufanya kazi mpaka ililopelekwa chelezoni mjini Mombasa, Kenya ambako matengenezo au marekebisho yaliyofanywa huko yaligharimu serikali Dola za Marekani 90,000.

Mpaka sasa hakujatolewa maelezo ya wazi ya nini hasa kilikosekana wakati wa ujenzi wa meli hata kulazimisha ipelekwe chelezoni kutumia fedha zaidi ndipo iweze kuanza safari za kibiashara.

Hivi kwa mazingira hayo, ambamo bado sijaona ushiriki wa wafanyakazi wa shirika hata kusukumiwa lawama na tuhuma za kuhusika kuharibu meli, hapajaonekana haja ya kufanywa uchunguzi wa kina kugundua wahusika wakuu waandamizi ufisadi mkubwa wa fedha za wananchi?

Written by
Jabir Idrissa

+255 774 226248

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Waliofariki ajalini Arusha kuagwa siku ya maandamano Chadema

Spread the loveMIILI ya watu 25 waliofariki dunia katika ajali iliyohusisha lori...

Habari za SiasaTangulizi

Serikali kuiburuzwa mahakamani ajali iliyoua 25 Arusha

Spread the loveMTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), imeitaka...

Habari za SiasaTangulizi

Samia atoa pole ajali iliyoua 25, kujeruhi 21 Arusha

Spread the loveRais Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu...

Habari MchanganyikoTangulizi

25 wafariki dunia katika ajali Arusha

Spread the loveWatu 25 wamefariki dunia papo hapo mkoani Arusha katika ajali...

error: Content is protected !!