Thursday , 2 May 2024
Home Habari Mchanganyiko Samia asikia kilio cha wachimbaji wadogo Songwe, leseni 37 zagawiwa
Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Samia asikia kilio cha wachimbaji wadogo Songwe, leseni 37 zagawiwa

Spread the love

Serikali ya Awamu Sita, chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imetekeleza ombi la siku nyingi la wachimbaji wadogo wilayani Songwe kwa kuwatengea eneo la uchimbaji na kuwakabidhi jumla ya leseni ndogo 37 zilizopo eneo la Kata ya Saza kutoka leseni hodhi namba RL0009/2014 iliyokuwa Kampuni ya Bafex Tanzania Limited. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Hayo yameelezwa leo  tarehe 23 Machi 2024 na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde alipofika eneo la Saza wilayani Songwe kukabidhi leseni 19 kwa wachimbaji wadogo wa Kikundi cha Songwe Gold Family (SGF) na wachimbaji wengine wadogo wadogo 18 huku mchakato wa kuendelea kutoa leseni zaidi ukiendelea.

“Nimefika hapa leo kwa maelekezo ya Rais Samia ambaye amenielekeza nije kuwakabidhi leseni zenu za wachimbaji wadogo mlizomuomba na kuwa mnakwenda kuwekeza mitaji mikubwa sasa na kuongeza mzunguko wa fedha zitokanazo na shughuli za madini kufikia zaidi ya trilioni moja,” amesema Mavunde.

Mavunde amesema pamoja na kwamba wachimbaji hao wanachimba kwa kubahatisha, kwa kipindi cha Julai, 2023 hadi Februari, 2024 wamezalisha kilo 729.6 zenye thamani ya Sh 101.06 bilioni na kueleza kuwa anaamini kwa kupatiwa leseni hizo hawatomwongusha  Rais kwa kuongeza uzalishaji na mapato yatokanayo na madini.

Amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha inaondoa ujanja ujanja kwenye shughuli za uchimbaji madini ambapo tayari imekwishatangaza kufuta jumla ya leseni na maombi 2648 ambazo hazijaendelezwa na zimekiuka taratibu za umiliki wa leseni za madini.

Mavunde ameendelea kusisitiza kwamba hatosita kuendelea kufuta leseni kwa wamiliki wote ambao wanakiuka taratibu za umiliki wa leseni za madini, ambapo ametoa mfano wa uwepo wa baadhi ya watu sita  tu wanaomiliki leseni zenye ukubwa wa zaidi ya ekari milioni 13.

Vilevile, Mavunde ameahidi kuwa baada ya Serikali kuwakabidhi wachimbaji wadogo leseni ndogo za uchimbaji, inakwenda kuweka utaratibu mzuri wa kukabidhi taarifa za utafiti wa eneo hilo kwa kikundi cha SGF na hivyo kumuagiza mkuu wa wilaya kuhakikisha kwamba  leseni tatu namba 10, 11 na 12 ziwe wazi ndani ya siku 14 ili kupisha maeneo hayo kutangazwa ili kupata uwekezaji mkubwa.

Awali, akisoma risala kwa Waziri Mavunde, Mwenyekiti wa Kikundi cha Wachimbaji wadogo cha Songwe Gold Family (SGF), Simon Ndaki amebainisha kwamba Kikundi chao kiliomba siku nyingi maeneo ya kuchimba na kupelekea kushindwa kuwekeza mitaji mikubwa kutokana na kukosa uhakika wa maeneo.

“Tunaahidi sasa kwamba tunakwenda kuwekeza mitaji mikubwa na kuhakikisha tunaongeza mchango zaidi wa mapato ya halmashauri na Pato la Taifa kwa ujumla,” amesema Ndaki.

Akieleza kuhusu masuala mbalimbali ya Wilaya ya  Songwe, Mbunge wa Songwe, Philipo Mulugo amemshukuru Rais Samia kwa kutatua changamoto hiyo iliyodumu kwa muda mrefu.

“Naomba upeleke shukrani za wachimbaji wadogo kwa Mhe. Rais na mueleze  kwamba wapo tayari kusaidia kurejesha fedha zaidi ya bilioni 72 zilizolipwa Bafex Tanzania Limited kwa uzalishaji mkubwa wa dhahabu,” amesema.

Naye, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Songwe, ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Solomon Itunda ameeleza kuwa zaidi ya asilimia 70 ya mapato ya wilaya yanatokana na shughuli za uchimbaji madini, na kuahidi kwamba ataendelea kushirikiana na wachimbaji wadogo kuhakikisha sekta ya madini inakua zaidi wilayani Songwe.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Chadema waendelea kulilia katiba mpya

Spread the loveCHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeendelea kudai upatikanaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema kumshtaki Rais Samia

Spread the loveCHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetishia kumfungulia kesi ya...

Habari za Siasa

Tume huru ya uchaguzi yatangaza uchaguzi mdogo Jimbo la Kwahani

Spread the love  TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi, imetangaza uchaguzi mdogo...

AfyaHabari za Siasa

Dk. Biteko aagiza utoaji huduma saratani usiwe wa kibaguzi

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko...

error: Content is protected !!