May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia: Nitateua yoyote bila kujali chama anachotoka

Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Spread the love

 

RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema katika serikali yake, atateua mtu yeyote mwenye uwezi kutoka chama chochote cha siasa ili kujenga umoja wa kitaifa. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Kiongozi huyo wa awamu ya sita, ametoa ahadi hiyo leo Ijumaa, tarehe 7 Mei 2021, akizungumza na wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam, katika ukumbi wa Mliman City.

Amesema kila Mtanzania anapaswa kuchangia ujenzi wa Taifa.

“Katika kujenga uchumi, kila Mtanzania anapaswa kuchangia katika ujenzi wa uchumi bila kujali, tofauti zetu za jinsia, rangi, kabila, dini na imani yako ya siasa. Mandhali ni Mtanzania na imani yako ya siasa uliyonayo lazima tuchangie kujenga uchumi wetu,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amesema, “kwa nini nasema hivyo, kwa sababu huko mbele katika kupanga safu za kujenga uchumi sitachagua. Mtanzania yeyote mwenye weledi na umahiri anayeweza kuleta manufaa katika Taifa, nitamuingiza afanye kazi.”

Rais Samia ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), amewaeleza wazee hao kwamba, hivi karibuni Serikali yake itafanya mabadiliko, hivyo kama wataguswa nayo kwa namna moja au nyingine, wajue ni kwa nia njema ya kuijenga Tanzania.

“Wazee wangu mtashuhudia mabadiliko, nia yake ni kuitengeneza na si kubomoa, mtakavyoona tunaleta mabadiliko katika nyanja mbalimbali mjue tuna nia njema kuijenga nchi na si kubomoa. Katika mabadiliko haya kijana wako akiguswa ujue tunafanya kwa nia njema na si mbaya,” amesema Rais Samia na kuongeza:

“Kwa hiyo hilo nalo katika kuleta umoja wa kitaifa, kila Mtanzania achangie. wote tutapangana kwenye safu ya kujenga nchi hii ilimradi mtu hana dosari za kimaadili na kiusalama.”

error: Content is protected !!