WAZEE wa Mkoa wa Dar es Salaam, wameiomba Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, ianzishe utaratibu wa kundi hilo kuwa na wawakilishi katika vyombo vya maamuzi, ikiwemo Mabaraza ya Madiwani na bungeni. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam.
Wito huo umetolewa leo Ijumaa tarehe 7 Mei 2021, na Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Mkoa wa Dar es Salaam, Salum Matimbwa, katika mkutano wao na Rais Samia, unaofanyika kwenye Ukumbi wa Mlimani City, mkoani humo.
“Ombi lingine ni uwakilishi wa wazee kwenye vyombo vya maamuzi, sisi wazee tunatambua katika vyombo ya maamuzi kuna makundi mbalimbali ya uwakilishi viti malaum, wanawake, vijana na walemavu. Lakini uwakailishi wa wazee haupo,” amesema Mzee Matimbwa.
Kiongozi huyo wa Wazee Dar es Salaam amesema “ombi letu kwako, wazee pia tunaomba kuwa na uwakilishi katika vyombo hivyo kama mabaraza ya madiwani, bunge na vyombo vingine ili tuwe na watu wa kutusemea matatizo yetu kwenye vyombo husika.”

Mwenyekiti huyo wa Wazee wa Dar es Salaam, amemuomba Rais Samia awawezeshe wazee kiuchumi, kwa kulijumuisha kundi hilo katika fedha za mikopo zinazotolewa na halmshauri kwa makundi maalum.
“Wazee tumekuwa tukikumbwa na changamoto mbalimbali za kiuchumi katika maisha yetu ya kila siku, ili kujikwamua kimaisha kwa kuwa serikali inatoa mikopo isiyo na riba kwa makundi maalum, kwa wanawake, walemavu na vijana kupitia halmashauri zetu,” amesema Mzee Matimbwa na kuongeza:
“Tunaomba na sisi tuongezwe katika kundi la nne ili nasi tunufaike na mikopo hiyo tuweze kujikimu na kujikwamua katika amisha yetu.”
Wakati huo huo, Mzee Matimbwa ameiomba Serikali iongeze juhudi katika kuwahudumia wazee waliotekelezwa na familia zao.
“Kumekuwepo na ongezeko la wazee waliotekelezwa na jamii zao kutokana na sababu mbalimbali, kama umasikini, magonjwa na kutowajibika kwa familia. Ombi letu kwako tunaomba serikali iendelee kuboresha makazi ya wazee yaliyopo na kuongeza mengine ili kuwatunza wazee waliotumikia Taifa,”amesema Mzee Matimbwa.
Pia, wazee hao wamemwomba Rais Samia kusimamia suala la kupata bima itakayowahudumia kwa matibabu yote.
“Tumepata kadi za msamaha wa bima, lakini wazee hatupati baadhi ya vipimo na dawa tukifika hospitalini. Tunaomba Mheshimiwa Rais, wazee tunapokuwa hospitalini, tupate vipimo na dawa zote kadri ya magonjwa yanayotusibu,” amesema
Leave a comment