May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia atoa msimamo ushirikiano Tanzania-Kenya

Spread the love

 

RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amewata watu kutolichonganisha Taifa hilo na Kenya. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Rais Samia ametoa wito huo leo Jumatano, tarehe 5 Mei 2021, akilihutubia Mabunge Mawili ya Kenya- Bunge la Taifa pamoja na Bunge la Senate kwa pamoja, jijini Nairobi nchini humo.

Kiongozi huyo wa Tanzania, amefanya ziara yake ya kwanza nchini Kenya jana Jumanne na kuihitimisha leo Jumatano, kufuatia mwaliko wa Rais wa nchi hiyo, Uhuru Kenyatta.

Akihutubia bunge hilo, Rais Samia amesema, mahusiano mema kati ya Kenya na Tanzania, yataendelea kuwepo.

“Yeyote anayefikiria kuleta uhasama baina yetu, ujumbe wao ni kwamba Tanzania na Kenya, tulikuwepo, tupo na tuatendlea kuwepo. Iwe kiangazi au masika Tanzania na Kenya tutaendelea kuwepo,” amesema Rais Samia.

Kutokana na mahusiano hayo, Rais Samia amesema, ameamua kufanya ziara nchini humo, ili kutafuta suluhu ya changamoto ziliopo baina ya mataifa hayo mawili.

“Nimekuja kuwaahidi kwamba, chini ya uongozi wangu, tutafanya kila linalowezekana kuimarisha ushirikiano kati ya nchi zetu mbili. Kama kuna linalo legalega au uhusiano wetu unasua sua, nimekuja Kenya ili kukazia yale ambayo yamelegalega na nimekuja kunyoosha yae ambayo yalikuwa yamepinda pinda,” amesema

Mbali na kuimarisha ushirikiano baina ya Kenya na Tanzania, Rais Samia amesema, nchi yake itahakikisha Jumuiya ya Afrika Mashariki inaimarika.

“Tanzania itaendelea kuwa jirani na rafiki kwa Kenya na mwanachama muadilifu wa kutumainiwa ndani ya EAC, jitihada zetu zitaelekezwa katika kuimarisha ushirikiano wetu ndani ya jumuiya yetu,” amesema.

“Kutafuta majawabu palipo na changamoto, kufufua fursa palipo na vikwazo, kuleta matumaini palipo na mashaka, tutafanya hivyo tukiamini wananchi wa EAC nafsi zetu zimefungamana nasi hatuna budi kufungamana,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amehimiza ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya katika masuala ya utalii.

“Utalii ni jambo lingine ambalo tunapaswa kushirikiana sana, kama nilivyosema ikolojia yetu inaingiliana, hivyo hivyo pia ukaribu wa vivutio vyetu vya utalii vinaingiliana, tunayonafasi ya kuneemeka pamoja ikiwa tutashirikiana katika sekta hii kuliko kushindana,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amesema “badala ya kunyang’anyana idadi ya watalii, busara inatutaka tuelekeze nguvu zetu kuhamasisha watalii kuongeza siku ambazo atazitumia nchini Kenya na Tanzania, kwa kufanya hivyo sote tutafaidika.”

error: Content is protected !!