September 25, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia ateua mawaziri na AG, watatu ‘out’

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan

Spread the love

RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko madogo ya baraza lake la mawaziri kwa kuteua mawaziri wanne na kuwaweka kando watatu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Uteuzi huo umetangazwa usiku wa leo Jumapili, tarehe 12 Septemba 2021 kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa na Jaffari Haniu, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu.

Mabadiliko hayo yamehusisha pia nafasi ya mwanasheria mkuu wa serikali (AG) ambapo ameteuliwa Jaji Kiongozi, Eliezer Feleshi kuchukua nafasi ya Profesa Adelardus Kilangi ambaye ameteuliwa kuwa Balozi.

Jaji Kiongozi, Eliezer Feleshi

Aidha, Rais Samia ameihamishia Idara ya Habari kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwenda Wizara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano na sasa itakuwa ikiitwa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia.

Mabadiliko hayo yameshuhudia ikiwarejesha tena kwenye baraza la mawaziri, Janaury Makamba, Profesa Makame Mbarawa anayerejea kwenye wizara aliyowahi kuhudumu ya ujenzi na uchukuzi.

Makamba kabla ya kutenguliwa katika utawala wa Hayati John Magufuli, alikuwa waziri wa muungano na mazingira.

Dk. Ashatu Kijaji ambaye aliwahi kuwa naibu waziri wa fedha na mipango sasa anakuwa waziri kamili wa habari, mawasiliano na teknolojia.

Dk. Ashatu Kijaji

Mabadiliko hayo yamewaweka kando mawaziri Dk. Faustine Ndugulile (mbunge wa Kigamboni), Dk. Merdard Kalemani (Chato) na Dk. Leonard Chamriho wa kuteuliwa na Rais.

Leo Jumapili, Dk. Chamriho alikuwa katika ziara na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ya kutembelea ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro.

Panga, pangua hiyo ya Rais Samia, imemjumuisha Dk. Stergomena Tax ambaye ameteuliwa kuwa waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

 

Anachukua nafasi ya Elias Kwandikwa aliyefariki dunia hivi karibuni jijini Dar es Salaam na mwili wake kuzikwa kwao, Ushetu, mkoani Shinyanga.

Dk. Tax ameteuliwa ikiwa ni takribani siku moja imepita baada ya Rais Samia, kumteua kuwa mbunge wa Bunge la Tanzania, Ijumaa ya tarehe 10 Septemba 2021 na siku hiyohiyo kuapishwa na Spika Job Ndugai, bungeni jijini Dodoma.

Dk. Tax alikuwa katibu mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), nafasi aliyoitumikia kwa miaka nane hadi Agosti 2021, alipomaliza muda wake wa uongozi.

error: Content is protected !!