RAIS wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amempongeza Rais Mteule wa Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC), kwa kuchaguliwa tena kuliongoza taifa hilo baada ya kumaliza muhula wake wa kwanza aliouanza 2018 hadi 2023. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).
Mkuu huyo wa nchi amekuwa kiongozi wa kwanza wa nchi mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kutoa salamu za pongezi kwa Tshisekedi, baada ya jana Jumapili kutangazwa mshindi wa kiti cha urais kwenye uchaguzi mkuu wa DRC uliofanyika tarehe 20 Disemba mwaka jana.
Kupitia ukurasa wake wa Twitter tarehe 31 Disemba 2023, Rais Samia aliahidi kumpa ushirikiano Rais Tshisekedi katika kuendelea kukuza mahusiano kati ya Tanzania na DRC.
“Pongezi za dhati kwa Rais Tshisekedi kwa kuchaguliwa tena kuwa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Natarajia kuendelea kufanya kazi pamoja katika kukuza uhusiano kati ya nchi zetu mbili na watu wetu,” aliandika Rais Samia.
Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na Mkuu wa Tume Huru ya Uchaguzi Congo (CENI), Denis Kadima, Rais mteule Tshisekedi, ameshinda baada ya kupata asilimia 73 za kura zilizopigwa.
Akitangaza matokeo hayo, Kadima amesema aliyekuwa mpinzani wa karibu na Tshisekedi, Moise Katumbi, amepata asilimia 18, wakati aliyeshika nafasi ya tatu, Martin Fayulu akiambulia asilimia Tano.
Leave a comment