RAIS Samia Suluhu Hassan, amelitaka Jeshi la Polisi lifute kesi za kubambikiza, ili kuondoa msongamano wa mahabusu gerezani. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).
Kiongozi huyo wa Tanzania ametoa agizo hilo leo Jumanne tarehe 18 Mei 2021, akifungua Chuo cha Ushonaji cha Polisi Kurasini, mkoani Dar es Salaam.
“Lakini pia niongee na Jeshi la Polisi kupunguza kesi za kubambikiza, kuna mlolongo mkubwa wa kesi za kubambikizwa. Sasa huku kupunguza mahabusu watapungua sababu wengi wapo wanasubiri kuhumikiwa, kesi haiendi ushahidi hakuna,” amesema Rais Samia.
Rais Samia amesema katika kukabiliana na changamoto ya mlundikano wa mahabusu, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), imefuta kesi 147 za kubambikiza.
“Nimezungumza na TAKUKURU wameweza kufuta kesi 147 ambazo waliwabambikizia watu mbalimbali huko, na nyie Jeshi la Polisi jikagueni kama mnazo za aina hiyo zifutwe ili tupunguze wingi wa mahabusu kwenye jela zetu,” amesema Rais Samia.
Awali, Inspekta wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro alisema jeshi hilo linashirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, kukabiliana na changamoto hiyo.
“Tuna mikakati mingi kuhakikisha uhalifu unapungua lakini kuna changamoto ya mlundikano wa mahabusu, tumeona ni changamoto tuko nayo lakini nikuhakikishe tunaendelea kufanya kazi na vyombo vya kijinai kuhakikisha yanapungua,” amesema IGP Sirro.

IGP Sirro amesema Jeshi la Polisi limeweka muda wa kikomo cha upelelezi, ili kuhakikisha haliwi chanzo cha kukwamisha uendeshaji kesi za mahabusu.
“Mfano makosa makubwa tumekubaliana lazima kwa miaka miwili, tuwe tumekamilisha upelelezi wa mashauri makubwa na mashauri madogo angalau miezi sita tuwe tumekamilisha upelelezi wa kesi,” amesema IGP Sirro na kuongeza:
“Hivyo nikuhakikishie rais, suala la mlundikano wa mahabusu tutaendelea kupunguza na suala la ucheleweshaji kesi, litaendelea kupungua kwa maana kwamba askari kwa mkosa madogo lazima miezi sita akamilishe jalada lake na makosa makubwa ifikapo miaka miwili lazima amekamilisha upelelezi.”
Leave a comment