RAIS wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Daktari Hussein Mwinyi, amewataka wafanyabiashara visiwani humo, kupunguza bei za bidhaa hususan vyakula, ili kuwasaidia wananchi wasiokuwa na uwezo wa kifedha. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).
Rais Mwinyi ametoa wito huo leo Jumanne, tarehe 31 Januari 2023, akizungumza na wafanyabiashara visiwani humo.
Ametoa wito huo baada ya bei za vyakula hasa mchele kupanda bei takribani mara mbili, kutoka wastani wa Sh.1,700 (2020) hadi kufikia 3,000 mwaka huu.
“Leo tunakaribia double price, inaumiza watu pamoja na bei nzuri iliyoko bara tukubali kukosa hiyo faida kwa kipindi hiki, tushushe bei ya ndani,” amesema Rais Mwinyi.
Katika hatua nyingine, Rais Mwinyi amewataka wafanyabiashara hao kuingiza mchele mwingi kwa wakati mmoja ili kudhibiti mfumuko holela wa bei, hususan katika kipindi hiki ambacho mwezi wa Ramadhani unatarajia kuanza.
“Najua kila mtu ana aina yake ya kufanya biashara, msaidiane tushushe mchele kwa wakati mmoja na katika nia moja tu ya kusaidia watu. Biashara inafanyika hata kama faida ni ndogo lakini tulenge kusaidia watu maana Zanzibar mchele ndiyo kila kitu,” amesema Rais Mwinyi.
Leave a comment