KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, imelitaka Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), kuajiri watangazaji au wasanii wenye vipaji badala ya kuajiri wenye elimu peke yake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Ushauri huo umetolewa leo Jumanne tarehe 31 Januari 2023, bungeni jijini Dodoma na Mbunge wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu, wakati akiwasilisha taarifa ya mwaka ya shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, kuanzia Januari 2022 hadi Januari 2023.
Mtaturu amesema kuwa, kamati hiyo inashauri TBC kuajiri wenye vipaji ili kukidhi ushindani wa soko la sasa.
“TBC kuna watangazaji au wasanii wenye vipaji vizuri lakini hawana sifa za kupata ajira kwa mujibu wa taratibu za Serikali na hali hiyo inasababisha shirika linashindwa kufanya ushindani na makampuni binafsi ya utangazaji ambayo yanazingatia vipaji,” amesema Mtaturu na kuongeza:
“Na kwa kuwa changamoto hiyo inasababisha kupunguza mvuto kwa wananchi ambao huvutiwa na vipaji hivyo, kwa hiyo basi, Bunge linashauri kwamba, Serikali iruhusu shirika la Utangazaji Tanzania – TBC kutoa ajira kwa watu wenye vipaji kulingana na matakwa ya soko.”
Leave a comment