KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, imeutaka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), iwachukulie hatua za kisheria wapangaji wake wanaodaiwa malimbikizo ya kodi, kwa kuwa wanakwamisha wakala huo kutekeleza miradi mingine.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Agizo hilo limetolewa leo tarehe 31 Januari 2023, bungeni jijini Dodoma na Mjumbe wa kamati hiyo, Miraji Mtaturu, wakati anawasilisha taarifa ya mwaka ya shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, kuanzia Januari 2022 hadi Januari 2023.
“Kuna changamoto ya wapangaji wa nyumba za TBA kutolipa kodi kwa wakati, kwa kuwa changamoto ya ulipaji wa kodi kwa wapangaji wa TBA inasabbabisha shirika kupata hasara na kushindwa kutekeleza miradi mingine, Bunge linashauri TBA ifuatilie wadaiwa sugu, iwachukulie hatua za kisheria bila kumuonea mtu aibu,” amesema Mtaturu.
Aidha, Mtaturu amesema kamati hiyo inaiagiza TBA kupeleka taarifa ya utekelezaji wa agizo kwa msajili wa hazina.
Katika hatua nyingine, Mtaturu amesema kamati hiyo inaishauri Serikali itoe fedha kwa TBA kwa wakati ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Leave a comment