Sunday , 28 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Rais mstaafu Karume: Nilishtuka uchaguzi 2015 kufutwa, awapa ujumbe CCM
Habari za SiasaTangulizi

Rais mstaafu Karume: Nilishtuka uchaguzi 2015 kufutwa, awapa ujumbe CCM

Aman Abeid Karume, Rais mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
Spread the love

 

RAIS mstaafu wa Zanzibar, Aman Abeid Karume amekumbushia kilichotokea katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kwamba matokeo ya uchaguzi huo yalifutwa pasina mazungumzo kufanyika. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).

Aidha, Kariume ambaye ni mtoto wa Hayati Abeid Aman Karume, mwasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar amesema, umefika wakati mazingira ya siasa yakaboreshwa yafanane na ya ulaya “kwani sote tuna haki sawa.”

Karume ambaye ni mwasisi wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) amesema hayo katika kongamano la kumbukizi ya Maisha ya Maalim Seif Sharif Hamad lililoanza juzi Ijumaa na kuhitimishwa jana Jumamosi, visiwani Zanzibar.

Kongamano hilo lililowakutanisha viongozi wa kisiasa na serikali, wa dini, wanazuoni, wanaharakati lilifunguliwa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Maalim Seif hadi anafikwa n amauti asubuhi ya tarehe 17 Februari 2021, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), jijini Dar es Salaam, alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar na Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo.

Rais mstaafu Karume akiwa madarakani pamoja na Maalim Seif wakati huo akiwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), waliongoza maridhiano na kuundwa na mwafaka wa kitaifa na kukubaliana uwepo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).

SUK ilipigiwa kura za wingi na Wazanzibar kwa zaidi ya asilimia 60 na kwa mara ya kwanza baada ya uchaguzi wa 2010, SUK ilianza kufanya kazi chini ya Rais Ali Mohamed Shein huku Maalim Seif akiwa Makamu wa Kwanza wa Rais, baada ya CUF kushika nafasi ya pili katika uchaguzi mkuu.

Rais mstaafu Karume akizungumza kwenye kongamano hilo, alirejea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 alisema uchaguzi wa mwaka 2010 ulikwenda vizuri lakini “2015 lilitokea sokomoko lingine balaa nchi hii.”

“Uchaguzi amekwisha, mtangazaji amekaribia kutangaza mara anaambiwa ajuwa. Tumetoka hapo ghasia zikaanza tena, vishindo na Maalim Seif akaomba mkutano na viongozi waliokuwa serikalini na mimi nikaalikwa,” anasema Karume, mtoto wa mwasisi wa mapinduzi ya Zanzibar, Hayati Aman Abeid Karume

Anasema, yeye alikuwa miongoni mwa walioshiriki kikao hicho ambacho Dk. Shein alikuwa mwenyekiti. Wengine kwenye kikao hicho alikuwa makamu wa pili wa Rais wa wakati huo, Balozi Seif Ali Iddi, Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi.

“Katika kikao kile, Maalim Seif alikuwa peke yake, sisi wengine sote CCM, Dk. Shein ndiye mwenyekiti, msaidizi wake Balozi Seif Ali Iddi, Mzee Mwinyi ambaye hakukaa sana.”

“Katibu mkuu kiongozi ndiyo alikuwa Katibu. Tukazungumza, tumekwenda tumekwenda, tukategemea kwamba mkutano utaendelea tutapata solution,” anasema Karume.

Maalim Seif Sharrif Hamad, Aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar

“Kukaja sherehe sijui ya mapinduzi, tupo uwanjani pale mara nasikia tangazo pale uchaguzi utarejea, mie nikashtuka, nikauliza mazungumzo yameisha, yakasema hayajaisha ila uchaguzi utarudiwa,” anasimulia

Anasema, baada ya taarifa hiyo, alichukua makablasha yake na kuyaweka sehemu moja mpaka sasa yapo na “baada ya pale tukarejea kule kuleeee, kila tukijaribu na mazungumzo hayakuendelea.”

“Wenzetu hawakuingia kwenye uchaguzi wa marudio lakini wakachukuliwa wapinzani sehemu mbalimbali ili waonekane wako kwenye serikali,” anasimulia Karume

Huku washiriki wa kongamano hilo wakimsikiliza, Karume anasema “pengine tungekuwa na uvumilivu kidogo tu, tukaendeleza mazungumzo yale tungekubaliana mambo fulani fulani na kuingia kwenye uchaguzi kwa pamoja.”

Kauli hiyo iliibuka miguno na kelele za hapa na pale na Karume akasema “ni vizuri kuwa wakweli na wawazi, kwa sababu mbele yetu tuna nchi na nchi ina watu na kila mtu ana haki sawa sawa na wewe. Marehemu Mzee Karume alikuwa anatuambia kila siku, tukizungumza masuala ya siasa kuwa hii siyo nchi yetu peke yetu.”

“Hii ni nchi yetu sote na sote tuna haki sawa sawa kwa sababu ni Republic siyo sultan na sote lazima tuwe wamoja, tuvumiliane, tushirikiane na sote tuna lengo letu ni kujenga umoja, sasa kwa vyovyote ukizungumzia umoja, ushirikiano niya CCM lakini siyo sera ya CCM peke yetu. Wapi imeandikwa, ni ya watu wote.”

“Hatujasema hii ni sera ya wana CCM pekee, hii ni ya wote sasa Maalim Seif naye alikuwa anaamini katika hili na sera hii. Tunakubaliana kwamba hili linatuunganisha sote,” anasema Karume.

Akihitimisha simulizi yake kumhusu Maalim Seif, anasema “namshukuru sana yule Mzee, kaka yangu kanizidi umri, lakini namshukuru sana kwa sababu pamoja sana na disappointment zote alizozipata katika siasa za maisha, hajakata tamaa, hajavunjika moyo na wala hajafika mahali akawaambia wafuasi wake basi au liwalo na lile.”

“Ameshika msimamo ule ule wa kutaka kujenga umoja kwa wananchi wa Zanzibar,” anasema

“Siku za mwisho mwisho za uhai wake, kuna mtu alisikika mtu anasema amemshukuru mwenyezi kwa kumjaali kusafiri katika barabara yake ya siasa.”

Hata hivyo, Karume amesema, barabara za ulaya ni nzuri zimejengwa vizuri tofauti na barabara “za kwetu sisi, mashimo mashimo tu. Na barabara ya siasa kwetu ni hivyo hivyo, kwa nini tusitengeneza barabara vizuri kama za ulaya, tunazungumza na kusalimia, wakati umefika tufanye hayo.”

Matokeo ya uchaguzi mkuu 2015, yalifutwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha na uchaguzi huo ulirejewa tena huku CUF wakiususia uchaguzi huo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mavunde aibana kampuni kutimiza masharti ya mkataba

Spread the loveWaziri wa Madini, Anthony Mavunde ameitaka Kampuni ya Xin Tai...

Habari za Siasa

Sauti ya Watanzania waeleza sababu za kuiunga mkono Chadema

Spread the love  KIKUNDI kinachojipambanua katika kupigania rasilimali na uhuru wa nchi,...

Habari MchanganyikoTangulizi

Jacob, Malisa waachiwa kwa masharti

Spread the love  JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam,...

Habari za SiasaKimataifaTangulizi

Tanzania, Somalia kuibua maeneo mapya ya ushirikiano

Spread the love  RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania na Somalia...

error: Content is protected !!