Wednesday , 1 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Rais Dk. Mwinyi amgusa Simai, “atakayejiuzulu aseme ukweli”
Habari za SiasaTangulizi

Rais Dk. Mwinyi amgusa Simai, “atakayejiuzulu aseme ukweli”

Spread the love

RAIS Dk. Hussein Mwinyi ameapisha mawaziri wapya aliowateua hivi karibuni huku akiasa kwa anayeamua kujiuzulu “aseme ukweli.” Anaripoti Jabir Idrissa, Zanzibar…(endelea).

“Kujiuzulu si jambo geni. Mawaziri wanajiuzulu kwa sababu ni suala la uwajibikaji… hizi nafasi si za mtu kukaa maisha. Jambo la muhimu ni pale mtu anapoamua kujiuzulu, kusema ukweli wa sababu za uamuzi aliochukua,” amesema Rais Mwinyi.

Ametoa ujumbe hu oleo Alhamisi baada ya hafla ya kuapisha mawaziri wawili wapya, mmoja aliyempa majukumu mapya, naibu mawaziri wawili aliowabadilisha na mmoja aliyempa dhamana nyengine.

Walioapishwa katika hafla iliyofanyika Ikulu ya Mnazimmoja, mjini Zanzibar, ni Mudrik Ramadhan Soraga anayekuwa Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale na Ali Suleiman Ameir aliyeteuliwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Ikulu).

Waziri mpya aliyeapishwa ni Shaaban Ali Othman, mwakilishi wa Jimbo la Mpendae, anayekuwa Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi.

Soraga anawakilisha Jimbo la Bububu wakati Ameir ni Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi, Jimbo la Pangawe, Wilaya ya Magharibi B, Unguja.

Waapishwaji wengine ni naibu mawaziri wapya Salha Mohamed Mwinjuma anayekuwa Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi na Zawadi Amour Nassor anayekuwa Wizara ya Maji, Nishati na Madini. Salha anayoka Viti Maalum kundi la Vijana mkoa wa Kusini Unguja wakati Zawadi anawakilisha Jimbo la Konde, Kaskazini Pemba.

Simai Mohammed Said.

Mwengine aliyeapishwa Naibu Waziri ni Juma Makungu Juma aliyehamishiwa Wizara ya Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais (Fedha na Mipango) kutoka Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi.

Makungu ni Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi, Jimbo la Kijini, Kaskazini Unguja.

Akizungumza baada tu ya kuwaapisha, Rais Dk. Mwinyi alisema kujiuzulu hutokea kwa njia mbili: Moja ni pale Waziri anapolazimika tu kuwajibika kwa makosa yaliyotokea kwenye sekta anayoisimamia, hata kama kosa lenyewe hakulifanya yeye.

Njia ya pili, anasema, ni pale kunapotokea kinachoitwa “mgongano wa maslahi” kutokana na uamuzi fulani uliofanywa na Serikali ambao yeye waziri atakuwa hakuuafiki ukiwa umemgusa kimaslahi.

Bila ya kumtaja kwa jina, lakini ikimaanisha anamlenga Simai Mohamed Said kwa kuwa ndiye aliyetangaza kujiuzulu tarehe 26 Januari, Rais Mwinyi alisema inapotokea serikali imeamua jambo fulani na Waziri wa sekta iliyoguswa akiwa ana maslahi, kujiuzulu ni muhimu ili kuonesha umeathirika  na uamuzi wa serikali.

“Sasa ni vizuri uamuzi wa kujiuzulu na ukaamua kutangaza, basi useme ukweli,” alisema.

Alifafanua kiasi akisema kama serikali imezuia kitu fulani kuagizwa, wewe Waziri hukuafiki uzuiaji huo, unaipata hoja ya kujiuzulu.

Hakutoa maelezo zaidi ya yale ya “kutupia” aliposema ikiwa sisi tumezuia biashara ambayo wewe una baa yako, na hukuafiki uzuiaji, basi unawajibika, lakini ueleze ukweli wenyewe.”

Simai alipojiuzulu alitaja alichosema “mazingira yasiyo rafiki” kuwa ni tatizo linalomkwaza kutekeleza majukumu yake na anaona anashindwa kumsaidia Rais kutekeleza yale aliyomteua kuyafanya.

Hakueleza undani wa hoja yake, lakini uamuzi wake ulikuja siku chache baada ya kuvieleza vyombo vya habari tatizo lililosababisha uhaba wa ulevi kwenye mahoteli makubwa na migahawa Zanzibar.

Alieleza kuwa maamuzi ya Bodi ya Vileo na Leseni ya Zanzibar, yamezua malalamiko na wadau katika biashara wamekuwa wakimtaka atafute ufumbuzi haraka lakini hapati ushirikiano alioutarajia licha ya jitihada zake.

Inajulikana Simai tangu hajaingia katika siasa na kugombea uwakilishi jimbo la Tunguu, Wilaya ya Kati, Unguja, ni mfanyabiashara na mwekezaji katika sekta ya utalii. Moja ya biashara zake ni kumiliki mgahawa maarufu wa Mercury, ulioko Forodhani, ndani ya Mji Mkongwe.

Kinachoelezwa kwa ndani ni uamuzi wa Bodi ya Vileo na Leseni kubadilisha waagizaji ulevi ikielezwa kuwa utaratibu wa kisheria haukufuatwa. Inadaiwa kuwa walioingizwa si wawekezaji wa Kizanzibari kama sheria inavyotaka.

Rais ameapisha watano aliowateua Jumamosi, lakini hajateua waziri wa kuziba pengo baada ya kumpa dhamana mpya Soraga aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji.

Mabadiliko madogo ya Baraza la Mapinduzi aliyoyafanya Daktari Mwinyi yamemtoa nje swahibu wake kisiasa Jamal Kassim Ali aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu. Jamal alisemekana kuwahiwa kwa kubwa alishatoa taarifa ya kuomba kujiuzulu.

Written by
Jabir Idrissa

+255 774 226248

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mavunde ataja malengo “Vision 2030”

Spread the loveWAZIRI wa Madini amesema dhana ya “Vision 2030” inakusudia kuiendeleza...

Habari za Siasa

Mavunde aomba bilioni 231.9 bajeti wizara ya madini

Spread the loveWAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde leo Jumanne amewasilisha hotuba ya...

Habari za SiasaTangulizi

Lissu amjibu Fatma Karume kuhusu Rais Samia

Spread the love  MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)...

Habari za SiasaTangulizi

Dk. Slaa: Watanzania iungeni mkono Chadema uchaguzi 2025

Spread the loveMWANASIASA mkongwe nchini Tanzania, Dk. Wilbroad Slaa, amewataka watanzania wakiunge...

error: Content is protected !!