March 4, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Prof. Ndalichako aendeleza makali yake

Prof. Joyce Ndalichako, Waziri wa Elimu

Spread the love

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amelitaka Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) kuvifungia vyuo visivyokidhi vigezo hasa vile vilivyowekwa chini ya uangalizi. Anaripoti Regina Kelvin…(endelea).

Prof. Ndalichako ametoa agizo hilo leo tarehe Agosti 9, 2018 jijini Dar es Salaam wakati akizindua baraza jipya la uongozi la NACTE.

“Mwaka 2017 vyuo 464 vilifanyiwa ukaguzi, 20 kati ya hivyo vilifungiwa baada ya kubainika havijakidhi vigezo, vyengine viliwekwa chini ya uangalizi huku vingine vikapewa muda wa kurekebisha mapungufu yake.

“Hivi vyuo vilivyo chini ya uangalizi mkiona havikidhi vigezo, vifungieni,” amesema na kuongeza;

“Anzieni hapo, msisite kufunga chuo chochote kiwe cha umma au binafsi msione huruma fungeni. Hatutaki kuwa na vyuo utitiri halafu havina ubora, tunataka tuwe na vyuo vinavyokidhi vigezo na kutoa wahitimu wenye elimu bora.”

Vile vile, Prof. Ndalichako amelitaka baraza hilo kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika vyuo vilivyosajiliwa na vitakavyosajiliwa ili kuhakikisha elimu inayotolewa kwa wahitimu inakidhi soko la ajira.

Katika hatua nyingine, Prof. Ndalichako amelitaka baraza jipya la NACTE kuongeza juhudi katika kufanya utafiti wa soko la ajira ili liweze kuwashauri wawekezaji wanaotaka kuanzisha vyuo kutoa mafunzo yanayokidhi soko la ajira.

Sambamba na hilo, ameishauri NACTE kutoa ushauri kwa wanaotaka kuanzisha vyuo, kutoa mafunzo kuhusu sekta zinazotoa ajira kwa sasa, hususani sekta ya kilimo, viwanda, madini na gesi.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi NACTE, Prof. John Kandoro amemhakikishia Prof. Ndalichako kwamba watatekeleza maagizo yake, akisema kuwa, baraza lake litaendelea kufanya tathimini ya ubora wa vyuo pamoja na kuendeleza elimu ya ufundi ili kufanikisha adhma ya serikali ya uchumi wa viwanda.

error: Content is protected !!