JESHI la Polisi Kanda Maalum Dar es salaam, limewakamata watuhumiwa mbalimbali wanaojihusisha na makosa mbalimbali ya kiuhalifu yakiwemo makosa ya kutumia madawa ya kulevya, anaandika Irene David.
Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda maalum ya Dar es Salaam, Lucas Mkondya, amethibitisha hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya Kanda Maalum ya Kipolisi ya Jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya vitu vilivyopatikana ni pamoja na silaha moja aina ya ‘shot gun’ na risasi tano, televisheni ya ‘flat screen,’ zimu sana na aina mbalimbali za madawa ya kulevya.
“Mnamo tarehe 16 Julai mwaka 2017 majira ya saa tatu usiku maeneo ya Pemba Mnazi Kigamboni, Jeshi la Polisi lilifanikiwa kukamata silaha moja ikiwa na risasi ndani ya magazine, ” amesema Mkondya.
Aidha Jeshi la Polisi limewakamata watuhumiwa wanne wakiwa kwenye bajaji yenye namba ya usajili MC 990 BLR rangi ya bluu,wakiwa na televisheni ‘flat screen’ mbili za inchi 52 modeli ya LG, simu saba ambapo simu tatu ni aina ya Nokia, simu moja ni ya ‘sony ericson,’ simu moja ya ‘blackberry,’ ‘iphone’ moja, kamera moja aina ya sony, ‘hard disk’ tatu, kompyuta mpakato nne, chaja mbili za simu , ‘card reader’ moja na nyaraka mbalimbali.
Mkondya amesema, Jeshi la polisi linaendelea na kufanya msako mkali na mpaka sasa limefanikiwa kuwakamata jumla ya watuhumiwa 200 kwa makosa mbalimbali yakiwemo makosa yanayohusiana na madawa ya kulevya, unyanganyi wa kutumia silaha, utapeli, wizi, kucheza kamari, kuuza pombe haramu na bhangi.
Mkondya amemaliza kwa kuwaasa Waanachi kuendelea kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi ili kuweza kutokomeza kabisa vitendo vya uhalifu nchini.
Leave a comment