BENKI ya NMB imekabidhi msaada wa vifaa mbalimbali 750 vya kujifungulia vyenye thamani ya Sh milioni 15.3 ikiwa ni utekelezaji wa dhamira ya benki hiyo kuinua afya ya uzazi katika Wilaya ya Kigamboni. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).
Vifaa vilivyotolewa na benki hiyo ni pamoja na, pamba kubwa, mpira ya kuzuia uchafu (disposable mackintosh), taulo za kike za wazazi, nyembe za kupasulia, vibana kitovu vya watoto, nguo za watoto, bomba za sindano, nyuzi za kushonea nk.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi msaada huo iliyofanyika Kigamboni jana, Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Dar es Salaam, Dismas Prosper alisema msaada huo umekusudia kuunga mkono juhudi za Serikali za kutoa huduma bora za afya ya uzazi huku akisisitiza kuwa msaada huo utachangia ustawi wa watu binafsi kwa ujumla, familia, na jamii ndani ya wilaya hiyo.
Prosper alibainisha kuwa benki hiyo imeipa sekta ya afya kipaumbele kibubwa kwenye mkakati kabambe wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSI) kwani inaamini kuwa afya bora ni chachu ya maendeleo endelevu.
“Benki ya NMB kwa miaka saba sasa imekuwa ikitenga asilimia moja ya faida baada ya kodi (PAT) kufadhili mipango mbalimbali ya maendeleo nchini kama sehemu ya dhamira yetu ya kusaidia maendeleo endelevu katika maeneo ambayo benki yetu inafanya kazi.
“Leo tunafuraha kukabidhi vifaa vya kujifungulia vyenye thamani ya shilingi milioni 15.3 na tunaamini juhudi zetu zitasaidia sana kuokoa maisha ya mama wajawazito na watoto wao wachanga,” alisema.
Katibu Tawala (DAS) wa Wilaya ya Kigamboni, Pendo Mahalu wakati wa hafla hiyo alisema wilaya yake mapema mwaka huu ilifanya tathmini ya mahitaji kwa mwaka iliyoongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Halima Bulembo na kubaini kuwa wilaya hiyo inahitaji vifaa takribani 8,500 vya kujifungulia kila mwaka kwa ajili ya kuhudumia wanawake wajawazito na watoto wao wachanga.
Alisisitiza kwamba msaada uliotolewa na Benki ya NMB umekuja wakati muafaka na kuihakikishia benki hiyo kuwa wilaya yake itatumia ipasavyo vifaa hivyo vilivyotolewa kwa manufaa ya wanawake wote wajawazito wenye uhitaji.
“Kama wilaya, uhusiano wetu na Benki ya NMB umeenda mbali zaidi ya kuwa washirika wa maendeleo kwani benki hii imekuwa bega kwa bega nasi kila tunapoihitaji. Afya bora inahitaji utoaji wa huduma za afya kwa wakati na kwa ufanisi.
“Tunashukuru sana kwa msaada huu na tunaamini vifaa hivi vya kujifungulia vilivyotolewa vitasaidia kuweka tabasamu kwa kina mama wengi wajawazito ambao mara nyingi wanalazimika kuingia gharama za ziada ili kununua vifaa hivi muhimu,” alisisitiza.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Kigamboni, Dk. Mohammed Mnyau alisema msaada huo utakuwa ukombozi mkubwa kwa wanawake wajawazito wilayani Kigamboni kwa kuwa vifaa vya kujifungulia ni gharama na kuishukuru benki hiyo kwa mchango wake.
“Wakati mwingine ukosefu wa vifaa vya kujifungulia unasababisha ucheleweshaji wa utoaji huduma usio wa lazima. Tunaamini kuwa baada ya kupokea vifaa hivi kutoka Benki ya NMB sasa tutawezesha kutoa huduma za papo hapo kwa wanawake wajawazito wenye uhitaji. Kwa wastani, hospitali yetu inapokea kati ya akina mama wajawazito 5000 – 10,000 kila mwaka,” Dk. Mnyau alisema.
Alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wadau wengine wa maendeleo wilayani humo kuendela kuchangia vifaa vya kujifungulia ili kuiwezesha wilaya yake kufikia malengo iliyojiwekea ya kukusanya vifaa 8,500 mwaka huu.
“Hadi leo, tumeweza kukusanya takriban vifaa 3,500 vya kujifungulia hivyo bado tuna upungufu wa vifaa 5,000 ilikufikia lengo letu la kukusanya vifaa vya kujifungulkia 8,500 mwaka huu.
“Napenda kuchukua fursa hii kutoa wito kwa kampuni zote zinazofanya kazi katika Wilaya ya Kigamboni kutungua mkono katika dhamira yetu nzuri ya kuokoa maisha mama na mtoto,” alisema.
Leave a comment