Sunday , 28 April 2024
Home Habari Mchanganyiko NGO’s zamuomba Samia airudishe Tanzania kwenye mpango Serikali wazi
Habari Mchanganyiko

NGO’s zamuomba Samia airudishe Tanzania kwenye mpango Serikali wazi

Spread the love

MASHIRIKA yasiyo ya kiserikali (NGO’s) 263 yanayotetea haki za binadamu, yamemuomba Rais Samia Suluhu Hassan, airejeshe tena Tanzania katika Mpango wa Ubia wa Serikali Huria (OGP), unaohamasisha uwazi na uwajibikaji serikalini. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Mashirika hayo chini ya mwamvuli wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) yametoa wito huo kupitia barua ya wazi waliyoandika kwa Rais Samia.

“Tunaomba ikupendeze kupokea barua hii ya wazi kutoka kwa watetezi wa haki za binadamu, kuhusu kujiunga tena OGP  yaani Open Government Partnership. Tumeamua kwa pamoja kufanya hivi kwa kuwa kwa kinywa chako, ulisisitiza kuwa serikali yako ni ya mazungumzo na tukiwa na chochote chenye kuhitaji mazungumzo tusisite kuomba nafasi ya kujadili na kuafikiana,” imesema barua hiyo iliyoandikwa na Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa.

Barua hiyo imesema kuwa, OGP ni utaratibu unaowasaidia viongozi wa nchi za kidemokrasia kuendesha nchi kwa urahisi huku misingi ya haki za binadamu na utawala bora ikizingatiwa.

Mashirika hayo kupitia barua ya wazi yamesema kuwa, katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Jakaya Kikwete, Tanzania ilijiunga na OGP na kupata mafanikio mengi, miongoni mwayo ikiwa ni kuongeza uwazi serikalini, kupitia njia mbalimbali ikiwemo uanzishwaji wa kamati tatu za waangalizi za Bunge zinazoongozwa na wabunge kutoka vyama vya upinzani.

Mafanikio mengine yaliyotajwa katika barua hiyo yaliyotokana na OGP, ni kuongeza ushiriki wa wananchi katika kufanya maamuzi yamambo yanayogusa moja kwa moja maslahi yao. Kuimarisha uadilifu na uwajibikaji katika utawala wa umma na teknolojia na ubunifu.

“Kwa heshima kubwa tunaomba kuishauri Serikali yako kujiunga tena na OGP kwa sababu mila, imani na mienendo mingi ya uongozi wako iko ndani ya mihimili ya OGP. Sababu za kujiunga na OGP mwaka 2011 kama ilivyoelezwa hapo juu bado ni halali na zinapita sababu zote zilizotolewa mwaka 2017 kwa njia isiyo rasmi na rasmi ya kujiondoa kwenye OGP.

“Nia ya Serikali katika kuleta mabadiliko chanya kisheria na kitaasisi nchini Tanzania chini ya usimamizi wako, kunaifanya Tanzania kuwa na sifa zote za kujiunga tena na OGP,” imeeleza barua hiyo na kuongeza:

“OGP imejengwa katika misingi mikuu ya utawala bora ambayo ni, uwazi, ushirikishwaji wa wananchi, uwajibikaji na uadilifu na teknolojia na ubunifu ambao unaonekana kuwa mwelekeo wa sasa wa uongozi wako.

“Mpango wa sasa wa Maendeleo wa Miaka Mitano unasisitiza juu ya ushirikishwaji na ushiriki wa wananchi katika programu mbalimbali za maendeleo. OGP ni chombo chenye nguvu cha kufikia vipaumbele vya nchi nzima kwa Serikali ya Tanzania na Asasi za Kiraia.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Mvungi aendesha kikao kazi cha wataalam wa Regrow

Spread the love  MKURUGENZI wa Idara Sera na Mipango Wizara ya Maliasili...

Habari MchanganyikoTangulizi

Jacob, Malisa waachiwa kwa masharti

Spread the love  JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam,...

Habari Mchanganyiko

Polisi wakanusha kufanya uzembe ajali iliyouwa mwandishi Ayo Tv

Spread the loveJESHI la Polisi limekanusha tuhuma zilizoibuliwa dhidi yake  kwamba limekawia...

Habari Mchanganyiko

Rais Samia kuzindua gazeti litakalotoa habari za wafanyakazi Tanzania

Spread the loveSHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), liko mbioni kufufua...

error: Content is protected !!