Sunday , 28 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Nape aihofia Chadema, ataka CCM ijipime kwa mikutano ya hadhara
Habari za SiasaTangulizi

Nape aihofia Chadema, ataka CCM ijipime kwa mikutano ya hadhara

Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Tekinolojia
Spread the love

 

WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema kitendo cha chama cha upinzani Chadema, kuanzisha mfumo wa usajili wanachama wake kidIgitali, kitaleta ushindani dhidi ya chama tawala (CCM). Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Nape ambaye aliwahi kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ametoa kauli hiyo leo Jumatatu, tarehe 17 Oktoba 2022, akihojiwa na Kituo cha Televisheni cha E, alipoulizwa, anaionaje nguvu ya Chadema iliyokuwa chini ya Katibu Mkuu, Dk. Wilbroad Silaa na ya sasa chini ya Katibu Mkuu, John Mnyika.

“Hawatatusumbua lakini wataleta ushindani. Nawaona wanafanya usajili kidigitali kuwafikia watu kule chini, hiyo kidogo italeta joto kwa sababu shida ya upinzani muda mrefu walikuwa wako hewani huku chini walikuwa hawapo, kwa hiyo wakirudi sie tunakwenda tunasafisha,” amesema Nape.

Nape amesema “usajili ni njia nzuri ya kuimarisha chama sababu huwezi kuwa na chama hewani lazima uwe na chama chini. Moja ya siri ya CCM ni kwamba kila ukihesabu nyumba 10 kuna balozi wetu pale. Unaweza mwambia balozi kati ya watu wako wangapi sio wetu anasema. Ndiyo maana ilikuwa rahisi kushinda, anasema katika nyumba 10 nyumba sita zetu, nne sio zetu tunaangalia tukaziombe au tuziache.”

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Samia Suluhu Hassan

Hata hivyo, Nape amesema CCM ina uwezo wa kubadilika kulingana na mazingira, hivyo Chadema hawatawasumbua.

Amesema, Makamu Mwenyekiti wa CCM , Abdulrahman Kinana amewekwa katika wadhifa huo kwa ajili ya kumsaidia Mwenyekiti wa chama hicho, Samia Suluhu Hassan, kukijenga chama kwa kuwa ana uzoefu utakaosaidia kukipa uhai chama hicho.

“Kimsingi tumemkabidhi jahazi atuvushe, yako mambo ambayo nadhani alipokuwa pembeni anajua. Tunaamini kwamba kutakuwa na mageuzi makubwa ndani ya chama chetu, tutakipa uhai tena msisahau tumekuwepo madarakani miaka 60, huo sio muda mdogo ni rahisi watu kuanza kuwachokeni kwa hiyo mnahitaji watu wa kufanya mabadiliko na sera,” amesema Nape.

Katika hatua nyingine, Nape ameipongeza hatua ya Rais Samia Suluhu Hassan, kuanzisha mchakato wa kurejesha mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, akisema mikutano hiyo inasaidia CCM kujipima na kujiimarisha zaidi, kuliko ilivyo sasa inapambana na vyama vya upinzani ambavyo vimefungwa mikono.

Zitto Kabwe kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo

“Sio tu kama mdau wa demokrasia, lakini kama mwana CCM wa kweli ninaamini kwamba mikutano ya siasa ingeimarisha CCM zaidi kuliko hali ilivyo, mimi ni kati ya wale tunaoamini toka mwanzo kabisa kwamba vizuri tufungue watu wafanye siasa. Kama unataka kujipima usijipime wakati mwenzako kafungwa mkono,”

“Nendeni mkashindane, mkajenge hoja isipokuwa jambo la msingi kuliko yote ambalo nadhani ni jambo la kuzingatia, Rais ameunda kikosi kazi kinaenda kutuletea namna bora ya kufanya kwa sababu pia hamuwezi kufanya siasa muda wote,” amesema Nape.

Amesema mikutano ya siasa itasaidia Serikali kupata maoni kutoka kwa wapinzani, yenye lengo la kuboresha utendani wake.

“Ninaimani kwamba mikutano na ushindani wa kisiasa una afya kwa nchi, demokrasia na kwa maendeleo yenyewe sababu mkiwa mnaongoza hivi wakati mwingine hamna anayewasema, hivi ni rahisi mkajisahau sababu ni binadamu. Mnaweza kufanya chochote lakini wakiwepo watu wanawasema hili jambo sio sawa mnarudi ndani mnakaa mnayabadilisha,” amesema Nape.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Askofu Shoo awataka ACT kupigania maslahi ya Taifa, wasikubali kuhongwa

Spread the loveALIYEKUWA Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri, Askofu...

Habari za Siasa

Biteko aagiza waajiri kudhibiti vifo mahali pa kazi

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mavunde aibana kampuni kutimiza masharti ya mkataba

Spread the loveWaziri wa Madini, Anthony Mavunde ameitaka Kampuni ya Xin Tai...

Habari za Siasa

Sauti ya Watanzania waeleza sababu za kuiunga mkono Chadema

Spread the love  KIKUNDI kinachojipambanua katika kupigania rasilimali na uhuru wa nchi,...

error: Content is protected !!