Saturday , 27 April 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Nani aweza kumuamini tena Prof. Lipumba?
Makala & UchambuziTangulizi

Nani aweza kumuamini tena Prof. Lipumba?

Spread the love

Na Saed Kubenea

PROF. Ibrahim Haruna Lipumba, anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, kuwa ndiye mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), ni kinyonga. Ana ndimi mbili.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, tarehe 21 Februari 2019, Lipumba amesema tofauti na alichokieleza Agosti 2017, katika mahojiano yake na kituo cha televisheni cha Clouds.

Alichokieleza Agosti 2017, sicho alichokieleza jana. Katika mazungumzo yake ya jana, Prof. Lipumba anasema, mgogoro wake ndani ya CUF na hata kujiuzulu kwake uongozi, kumetokana na msimamo wa Maalim Seif Shariff Hamad, “kung’ang’ana na Muungano wa Mkataba.”      

Prof. Lipumba anasema, msimamo huo wa Maalim Seif, ambaye ni katibu mkuu wa chama hicho, ni kinyume na masharti ya usajili wa vyama vya siasa.

Aidha, Prof. Lipumba anasema, hatua ya Maalim kutaka Muungano wa Mkataba, itasababisha chama hicho kufutiwa usajili.

Lakini katika mahojiano yake na Clouds, Prof. Lipumba alisema, “niliamua kujiuzulu kwa sababu niliona si sahihi kwa Lowassa (Edward Lowassa), kuingia ndani ya Ukawa na kugombea urais.”

Akakana pia kuwa ufisadi siyo mfumo, bali ni mtu binafsi. Akataka wananchi kupambana na ufisadi wa mtu binafsi, badala ya mfumo unaosababisha ufisadi.

Prof. Lipumba alitoa kauli hiyo, kuafuatia Maalim Seif kuhojiwa na kituo hicho na kusema, anayesababisha mgogoro ndani ya CUF, “ni Prof. Lipumba akisaidiwa na serikali.”

Alisema, ni Prof. Lipumba aliyemtafuta Lowassa kumshawishi kujiunga na UKAWA kwa lengo la kuwa mgombea urais. Alisisitiza, “nina ushahidi wa hili.”

Alimtuhumu kuwa msaliti. Akasema, ni bora kuketi meza moja na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuliko kuzungumza na Prof. Lipumba. Tujadili:

Kwanza, ni Prof. Lipumba aliyetangaza hadharani kumsimamisha kazi, Maalim Seif. Akamteua Magdalena Sakaya, kuwa kaimu katibu mkuu.

Alidai kuwa amechukua uamuzi huo baada ya Maalim Seif kushindwa kutimiza majukumu yake.

Akawaambia waandishi wa habari – tarehe 28 Machi 2017 – kuwa Maalim  Seif amekaidi wito wake wa kumtaka kufika Buguruni, kusimamia mikutano ya Kamati Tendaji, kujadili masuala ya chama hicho.

Akatangaza kuwafuta kazi wakurungezi wote kutoka Zanzibar akiwemo Salim Bimani, mkurugenzi wa habari na Uenezi; Abdallah Bakar Khamis, mkurugenzi wa fedha na uchumi na Pavu Juma Abdallah, mkurugenzi wa haki za binadamu.

Wengine ambao walitangazwa kufutwa kazi pamoja na Maalim Seif, ni Mahima Ali Mahima, katibu mtendaji JUVI-CUF; Yusuph Salim, naibu mkurugenzi ulinzi na usalama na Omar Ali Salehe, mkurugenzi mipango na uchaguzi.

Akamtaarifu mshirika wake wa karibu katika mradi wa kuangamiza CUF, Jaji Mutungi, juu ya hatua hiyo. Naye Mutungi akabariki kusimamishwa kazi Maalim Seif.

Uamuzi huo wa Prof. Lipumba na genge lake wa kudai amemsimamisha kazi Maalim Seif, ndio uliotumika kuhalalisha haramu ya kupitisha majina Mohammed Mnyaa, Thomas Malima na Sonia Magogo, katika orodha ya wagombea wa ubunge wa Afrika Mashariki.

Katika uchaguzi huo, Bunge liliridhia chama hicho kuwa na wagombea wanne wa ubunge, kinyume na kanuni za Kudumu za Bunge na mkataba wa uundwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

CUF iliwasilisha jina moja tu – la Twaha Taslima – kuwa ndiye mgombea wake katika uchaguzi huo.

Barua ya utambulisho wa Taslima iliandikwa na Maalim Seif Sharif Hamad, tarehe 21 Machi mwaka huu. Ilikuwa na Kumb. Na. CUF/HQ/KM/005/02/ 2017.

Lakini Sakaya alijitambulisha na mpaka sasa anaendelea kujitambulisha kuwa kaimu katibu mkuu wa chama hicho.

Prof. Lipumba hajasema, ikiwa anamtambua Maalim Seif kuwa katibu mkuu, kwa nini Sakaya bado anamtambulisha na kujitambulisha kwa wadhifa wa kaimu katibu mkuu?

Nani aliyemkaimisha Sakaya nafasi hiyo? Kwa nini amekaimishwa wakati mwenye nafasi yake bado yupo?

Pili, yawezekana Lipumba amesahau. Lakini kumbukumbu bado zipo, kwamba ni yeye aliyehubiri kwa miaka nenda rudi, Muungano wa Mkataba; na au muundo wa serikali tatu.

Hata ndani ya Bunge Maalum la Katiba, ni Lipumba, aliyekuwa kinara mkuu wa kutaka muundo huo. Je, mbona CUF haikufutwa wakati huo? Ni lini kuhubiri Muungano wa Mkataba kumegeuzwa jinai ya kisiasa?

Lakini si hivyo tu: Hata Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba, ilijadili suala la Muungano wa  Mkataba kwa uwazi na shirikishi. Haikufutwa. Haikukemewa. Rejea ripoti ya Tumen a randama zake.

Prof. Lipumba angekuwa mkweli angeeleza haya. Lakini kwa sasa hawezi kusema. Hana uhuru na utashi wa kusema ukweli.

Lipumba wa sasa, ni bingwa wa kubadilisha kauli. Hapa aweza kuzungumza hili, pale akazungumza lile. Hawezi tena kuaminika.

Wengi waliofanya naye kazi, sasa wanamfahamu kuwa ni mbinafsi, mchonganishi, msaliti na msahaulifu.

Anataka kuvuna kwa lisilo la haki na kwa dhamira chafu. Hii ndio taswira aliyojijengea tokea Agosti 2015 alipojiuzulu wadhifa wake wa uenyekiti.

Ndio maana hawezi kueleza anawezaje kumtambua Maalim Seif kuwa katibu mkuu? Ametumia kikao gani kumrejesha? Nani alimsimamisha? Alitumia katiba ipi?

Kwa maneno haya, hata wasio na macho wameanza kuona kilichosababisha machozi mapya ya Prof. Lipumba.

Kwamba, ni hatua ya Maalim Seif kujiimarisha kisiasa Bara. Ni hatua ya wanachama na viongozi kung’amua kuwa Lipumba na kibaraka wa serikali.

Katika mazingira hayo, nani sasa aweza kumuamini tena Prof. Lipumba? Hakuna.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

Habari za SiasaTangulizi

Mpwa wa Magufuli mbaroni kwa kusambaza picha za utupu

Spread the loveJESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata...

Habari za SiasaTangulizi

Shibuda amlima waraka mzito Bulembo

Spread the loveMKONGWE wa siasa nchini, John Shibuda amemshukia kada maarufu wa...

error: Content is protected !!