May 17, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Dk. Mayrose achukua fomu urais Chadema, aahidi chakula na mishahara bora

Dk. Myrose Majinge, amechukua fomu ya kugombea Urais wa Tanzania, kupitia Chadema

Spread the love

DAKTARI Mayrose Majinge, amechukua fomu ya kugombea Urais wa Tanzania, kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Dk. Majinge amekabidhiwa fomu hiyo leo Jumanne tarehe 7 Julai 2020 na Reginald Munisi, Mkurugenzi wa Uchaguzi Chadema, katika Ofisi za Makao Makuu ya Chadema, Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Dk. Majinge amekuwa mwanamke wa kwanza na mwanachama wa pili wa Chadema, kuchukua fomu hiyo tangu shughuli hiyo ianze tarehe 4 Julai 2020 na litahitimishwa tarehe 19 Julai, 2020.

Wa kwanza kuchukua fomu hiyo ni Tundu Lissu, aliyechukua fomu Jumamosi tarehe 4 Julai 2020, kupitia wakala wake David Jumbe.

         Soma zaidi:-

Akizungumza baada ya kuchukua fomu hiyo , Dk. Majinge  ametaja  mambo kadhaa ambayo atayafanyia kazi endapo atachaguliwa na Chadema kugombea nafasi hiyo, kisha kupata ridhaa ya wananchi kuwa rais wa Tanzania.

Dk. Majinge amesema, endapo atapata ridhaa hiyo, atajenga mfumo imara na madhubuti  wa uongozi wa taifa, kwa ajili ya maslahi ya kizazi cha sasa na vijavyo.

Amesema ahadi yake kwa Watanzania ni kuwezesha upatikanaji wa katiba ya wananchi na tume huru ya uchaguzi kwa ajili ya kulinda haki na wajibu wa kila Mtanzania, pamoja na kudhibiti utawala wa kibabe.

“Nikifanikiwa kuwa rais, ahadi yangu kwa Watanzania ni kuwezesha mahusiano mazuri ya kimataifa yenye kuleta tija kwa Tanzania,” amesema Dk. Majinge.

Amesema endapo atafanikiwa kuwa Rais wa Tanzania, ataboresha utawala wa sheria kwa kuondoa sheria kandamizi na kuhakikisha taifa lina sheria zinazozingatia haki na utu kwa wote.

“Ahadi yangu ni kuwezesha kila Mtanzania kuwa na uhakika wa chakula na matibabu, kupata elimu yenye kujenga maarifa na uwezo mkubwa wa kufikiri ili kutumia fursa zilizopo kuishi kwa uhuru na furaha. Kuwezesha uwepo wa ajira kwa mujibu wa kila fani na taaluma ya Mtanzania,” ameahidi Dk. Majinge.

Wakati huo huo, Dk. Majinge amesema, ameamua kugombea nafasi hiyo, ili kuboresha mfumo wa madaraja ya mishahara ya wafanyakazi wote wa taasisi za umma na binafsi, ili yaweze kukidhi mahitaji ya maisha.

“Nitawezesha mazingira rafiki na yenye kwa watu wanaoshughulikia kilimo, ufugaji na viwanda. Kuboresha utalii, kuweka mazingira mazuri katika biashara ya madini kwa wazawa na wawekezaji wa nje,” amesema Dk. Majinge.

Pia, Dk. Majinge ameahidi kuwawezesha raia wa Tanzania wanaoishi nje ya nchi kuwa na uraia pacha.

“Hizi ni ahadi zangu kwa Watanzania kuhusu mambo ya msingi niliyoyaandaa kwa mujibu wa taaluma yangu. Endapo chama kitanipitisha nawaomba Watanzania wote bila kujali itikadi zetu, watuunge mkono Chadema ili kuwezesha ahadi nilizotoa leo ziwe kweli,” amesema Dk. Majinge.

error: Content is protected !!