Spread the love

KATIKA jitihada za kuboresha elimu Benki ya Mwalimu imeingia mikataba na wamiliki wa shule na vyuo mbalimbali nchini ili kutoa mikopo ya masharti nafuu kwa wanafunzi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Aprili 6, 2022 Mkuu wa Kitengo cha Biashara na Masoko, Letisya Ndongole amesema mikopo hiyo itawanufaisha wazazi walioajiriwa kwenye taasisi za umma na zile binafsi pamoja na wanafunzi wanaojiendeleza wakiwa kazini.

“Huduma hii tumeiita Ada Chap Chap, itakayoongeza thamani na kuwajengea uwezo wamiliki wa shule ili mikopo iwe na tija kwao”

Amesema kuwa wabia kwenye huduma hiyo ni pamoja na:- Eag High School-Bagamoyo, City College of Health and Allied Sciences kampasi ya llala Goba (Mount Ukombozi), Covenant Institute of Accountancy and Technology -Kurasini Covenant Financial Consultants kwa wanataaluma wa uhasibu yaani CPA na Institute Heavy Equipment and Technology – Kijitonyama.

Amesema Benki hiyo inalenga kutoa huduma za kifedha kwenye taasisi za kielimu na wadau mbalimbali wa elimu.

“Mwalimu Benki imelenga ikolojia ya elimu kwa wanafunzi kwenye vyuo vya elimu, Walimu, Shule, Taasisi za elimu, Wizara ya Elimu, TAMISEMI, Wafanyakazi wa Umma na Taasisi binafsi na wadau wote wanaotoa huduma kwenye sekta ya elimu (mfano watengeneza chaki, samani za mashuleni na vifaa vya shule” amesema Ndongole.

Ndongole amesema benki hiyo yenye vituo 9 sehemu mbalimbali nchini na matawi mawili jijini Dar es Salaam itatoa huduma hiyo ambayo pia itakuwa bima kwa mteja atakayepa ulemavu au kifo.

“Benki yetu mpaka sasa ina matawi mawili yaliyopo Dar es salaam (Samora na Mlimani) na tunavyo vituo vya huduma 9 (Morogoro, Mbeya, Mwanza, Dodoma, Arusha, Rukwa, Kigoma, Mtwara na Arusha).

Matarajio yetu ni kuwa na vituo hivyo katika mikoa yote ifikapo mwaka 2025” amesema Ndongole.

Amesema benki hiyo imeandaa mkakati wa miaka mitano wenye lengo la kuboresha huduma zenye ubunifu kwa wateja wake.

“Moja ya maeneo yaliyopewa kipaumbele ni kuwa na bidhaa zinazolenga moja kwa moja mahitaji ya walimu, watumishi wa Umma, taasisi binafsi katika kujiinua kiuchumi na kuleta tija kwenye jamii”

Ndongole amesema benki hiyo imelenga utoaji wa huduma za kibenki ambazo ni rahisi, salama na zinazopatikana popote na wakati wowote kwa njia za kidijitali ikiwa ni Pamoja na Mwalimu Mobile, Mwalimu Wakala na Mwalimu visacard.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *