July 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Msukuma: Mbowe alipa-miss Ikulu

Spread the love

MBUNGE wa Geita Vijijini, Joseph Msukuma (CCM) amesema sio wanawake tu wanaofurahia utendaji wa Rais Samia Suluhu Hassan bali hata wanaume wanamfurahia. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Amesema hata vyama vya upinzani pia vimeufurahia ndio maana katika siku za karibuni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ameshaenda Ikulu zaidi ya mara tano.

“Hebu angalia leo Mbowe anaongoza kwenda ikulu, najua alipa-miss sana lakini amepata nafasi ya kuingia na kutoka zaidi ya mara tano, hongera sana mama Samia.

Msukuma ametoa kauli hiyo leo tarehe 26 Mei, 2022 wakati akichangia hoja ya Mbunge wa Viti Maalumu CCM, Zainab Athuman Katimba (CCM) ambaye aliwasilisha hoja hiyo na kuwaomba wabunge kumuunga mkono kupitisha azimio la kumpongeza Rais Samia kwa kutwaa tuzo huko nchini Ghana.

Jana tarehe 25 Mei 2022, mwaka huu Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ilimtunuku Rais Samia tuzo ya Babacar Ndiaye- 2022 kutokana na mafanikio yake kwenye ujenzi wa barabara wakati huohuo gazeti maarufu la Time la tarehe 24 Mei 2022 nalo likamtaja katika orodha ya viongozi 100 wenye ushawishi duniani.

Msukuma amesema anaifananisha tuzo hiyo na ligi ya Tanzania baada ya kuichukua kutoka Nigeria ambayo ilikuwa inaishikilia.

“Kwamba tumemnyang’anya Nigeria ambaye alikuwa na tuzo hiyo, ni sawa Tanzania tu tunatarajia kumnyang’anya mnyama very soon.

“Ningemuomba Rais Samia huko aliko anisikilize, najua atakuja, nimkaribishe sana Mwanza nimpe zawadi ya kitanzania. Aliyopewa kule ni tuzo aje tumpe mnyama keshokutwa tunamchinja apate zawadi,” alisema Msukuma.

Baada ya michango ya wabunge hao, Spika wa Bunge, Tulia Ackson aliwahoji wabunge kama wanaliridhia au lah na wabunge wote kwa pamoja wakalipitisha.

Spika Tulia alieleza kufurahishwa na umoja wa wabunge hao na kueleza kuwa hii ni mra ya kwanza kwa hoja kupitishwa kwa kauli moja na wabunge wote bila kujali wa vyama vya upinzani.

error: Content is protected !!