Tuesday , 21 May 2024
Home Habari Mchanganyiko Taasisi yaanzisha mafunzo kuwanoa wadau wa mawasiliano nchini
Habari Mchanganyiko

Taasisi yaanzisha mafunzo kuwanoa wadau wa mawasiliano nchini

Mratibu wa mafunzo kutoka Taasisi ya Mahusiano na Mawasiliano ya Umma nchini Tanzania (IPRT), Evarist Ngalimuwili akizungumza na waandishi wa habari pamoja na wageni waalikwa wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa mpango huo. Wengine ni pamoja na Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited, Bakari Machumu (kulia) na Katibu Mtendaji wa Chemba ya Madini Tanzania (TCM) Mhandisi Benjamin Mchwampaka (kushoto)
Spread the love

TAASISI mpya ya Mahusiano na Mawasiliano ya Umma nchini Tanzania (IPRT) imetangaza hatua kutoa mafunzo kuhusu mawasiliano ya kimkakati mahususi kwa watendaji wakuu, maofisa mawasiliano, maofisa utumishi pamoja na maafisa mbalimbali katika mashirika. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Akizungumza katika hafla fupi ya uzinduzi wa taasisi hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam leo tarehe 26 Mei, 2022 na kuhudhuriwa na wadau kutoka taasisi mbalimbali pamoja na vyombo vya habari, Mratibu wa mafunzo kutoka IPRT, Evarist Ngalimuwili amesema wazo la kuanzishwa kozi hiyo linachagizwa zaidi na uwepo wa changamoto katika eneo la mahusiano na mawasiliano ya umma kimkakati miongoni mwa taasisi mbalimbali hapa nchini.

Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited, Bakari Machumu (Kulia) akizungumza na waandishi wa habari pamoja na wageni waalikwa wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa mpango huo.
Wengine ni pamoja na Mratibu wa mafunzo hayo kutoka IPRT, Evarist Ngalimuwili (katikati) na Katibu Mtendaji wa Chemba ya Madini Tanzania (TCM) Mhandisi Benjamin Mchwampaka (kushoto)

Kwa mujibu wa Ngalimuwili, katika kufanikisha mpango huo, taasisi hiyo imejipanga kushirikiana na taasisi mbalimbali zinazotambulika kwa weledi katika ufundishaji wa masuala hayo zikiwepo za ndani na nje ya nchi, sambamba na kutumia wahariri wabobevu kwenye masuala ya mawasiliano na mahusiano ya umma katika utoaji wa kozi hizo.

“Mpango huu utahusisha ushirikiano baina yetu na Chuo Kikuu cha Daystar cha nchini Kenya ambao ni wabobevu katika masuala haya na kwa kuanzia tunatarajia kuanza na kozi mahususi kwa watendaji wakuu wa mashirika na taasisi mbalimbali, maofisa mawasiliano na mahusiano ya umma, maofisa utumishi pamoja na maafisa mbalimbali katika mashirika hayo kisha baadae tutahusisha wanahabari kutoka makampuni ya habari, wakiwemo wanafunzi kutoka vyuo vikuu.’’amesema Ngalimuwili.

Amezitaja kozi ambazo zitatolewa kuwa ni pamoja na programu za mawasiliano ya kimkakati kwa taasisi na mashirika kama vile Mawasiliano ya Biashara, mawasiliano wakati wa mgogoro (Crisis Communication), Usimamizi wa Chapa, Mawasiliano fanisi, Mawasiliano binafsi, mawasiliano ya kitaasisi sambamba na kozi nyingine zinazolenga kujenga ujuzi bora kwa wadau wa mawasiliano.

Katibu Mtendaji wa Chemba ya Madini Tanzania (TCM) Mhandisi Benjamin Mchwampaka (Kushoto) akizungumza na waandishi wa habari pamoja na wageni waalikwa wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa mpango huo. Wengine ni pamoja na Mratibu wa mafunzo hayo kutoka IPRT, Evarist Ngalimuwili (katikati) na Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited, Bakari Machumu (kulia)

Aidha, ili kuhakikisha taarifa zinazohusu sekta mbalimbali za kitaaluma zinaripotiwa kwa weledi na utashi mkubwa, Ngalimuwili amesema taasisi hiyo pia imeandaa mafunzo mahususi kwa wanahabari yakilenga kuwajengea uwezo katika kutoa taarifa zinazohusu nyanja hizo ikiwemo uchambuzi wa taarifa za fedha na taarifa za mahakama.

Nyingine ni habari za michezo na uchambuzi, taarifa zinazohusu sekta ya madini, mafuta na gesi, kilimo na mifugo, benki na bima, afya, ripoti za mazingira na Uchumi wa Bluu unaohusisha bahari, maziwa, mito, uvuvi, usafiri wa baharini na utalii.

“Lengo ni kuwajengea uwezo zaidi waandishi wa habari hapa nchini ili kuhakikisha habari zinazotolewa katika sekta mbalimbali zinaandaliwa kwa weledi wa hali ya juu na kwa usahihi” amesema

Ameongeza kuwa amefurahishwa kusikia mafunzo hayo ya msingi yataendeshwa kwa kushirikisha wataalamu na wakufunzi kutoka sekta husika.

Katika hatua nyingine inayolenga kuwezesha upatikanaji wa taarifa sahihi na za kuaminika katika maeneo ya Mahusiano na Mawasiliano ya Umma, Mawasiliano ya Kibiashara na Masoko pamoja na Uongozi na Utawala, Ngalimuwili amesema taasisi hiyo pia imejipanga kutambulisha chapisho maalum linalotambulika kama Reputation Today litakalo kuwa pia na agenda kuu ya kuthibitisha weledi katika eneo la mawasiliano.

Akizungumzia hatua hiyo Katibu Mtendaji wa Chemba ya Madini Tanzania (TCM) Mhandisi Benjamin Mchwampaka amesema ujio wa mkakati huo umekuja katika kipindi ambacho taifa linahitaji kuwa na waandishi wabobevu katika maeneo mbalimbali ya kimkakati ikiwemo eneo la madini ili taarifa zinazotolewa ziwe na tija kwa wananchi.

“Tukiwa kama wadau wa sekta ya madini tumeguswa sana na ujio wa mafunzo haya si tu kwa ajili ya mawasiliano yetu sisi kama taasisi bali pia tunahitaji kuona waandishi wakipata mafunzo haya muhimu.

“Sekta ya madini inahusisha uwekezaji mkubwa hivyo hata aina ya uandaaji wa taarifa zake unahitaji umakini na weledi mkubwa. Uwepo wa waandishi waliofundishwa vema kuripoti habari za madini utatusaidia sana kama taifa,’’ amesema

Akizungumzia hatua hiyo, Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited, Bakari Machumu amesema ni muhimu kwa wanahabari wote kuendelea kujifunza ili kujijenga taaluma kwa maisha yao yote ya kuhudumu sekta hiyo sambamba na kubuni mbinu mpya za kuendesha mambo katika tasnia hiyo inayokwenda kwa kasi huku ikipokea mabadiliko mapya kila siku.

“Mambo mengi yanabadilika katika tasnia yetu hivyo kuna haja ya kujifunza na kupanua uwezo wetu na kuwa na uelewa mpana kila wakati,” amesema.

Amesema mpango huo utakuwa sehemu muhimu katika kukuza na kuendeleza sekta ya mawasiliano nchini na juhudi za kudumisha tasnia hiyo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari Mchanganyiko

Waziri aipongeza NBS kwa mafanikio

Spread the loveNaibu Waziri wa Fedha, Hamad Chande amepongeza Ofisi ya Taifa...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Balozi Nchimbi aonya maofisa utumishi kuacha uonevu

Spread the loveKatibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Balozi Kasike ateta na mjumbe wa FRELIMO

Spread the loveBalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Msumbiji, Phaustine...

Habari MchanganyikoKimataifa

Zuma akwaa kisiki, mahakama yamzuia kuwani urais

Spread the loveMahakama ya katiba nchini Afrika Kusini, katika uamuzi wake imesema...

error: Content is protected !!