MWENYEKITI wa Chama cha Tanzania Labour Party, (TLP) Augustine Lyatonga Mrema amesema, katika uchaguzi mkuu mwaka 2020 chama chake hakitaweka mgombea wa Rais badala yake watampigia kura mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais John Magufuli. Anaripoti Hamis Mguta, Dar es Salaam … (endelea).
Mrema ameyasema hayo leo Ijumaa tarehe 5 Juni 2020 wakati akieleza maandalizi ya chama chake kuelekea uchaguzi mkuu.
Ameeleza kwa yote yaliyofanywa na rais huyo wa Tanzania ambaye anaelekea kumaliza miaka yake mitano ya awamu ya kwanza ya urais wake yanatosha kumfanya apewe nafasi ya kuongoza tena miaka mitano ijayo.
“Sina sababu ya kueleza sifa za Magufuli kwasababu tumeshaelezana, hatuweki mgombea urais sisi tutagombea ubunge na tutashindana na wenzetu, hatuungi mkono wagombea wa ubunge wa CCM.”

“Piga ua galagaza tutahakikisha Rais Magufuli anashinda kwenye uchaguzi huu, tutazunguka nchi nzima kufanya kampeni, wale wabunge wa CCM wanaompinga tutahakikisha tunasimamisha wagombea na kama watakuwa ni wazuri watashinda kama sio wazuri watashindwa,” amesema.
Ameeleza kuwa uamuzi huo umefikiwa na mkutano mkuu wa chama hicho uliofanyika tarehe 9 Mei 2020 na kuafiki kuwa watampigia kura na kumfanyia kampeni nchi nzima.
Hivi karibuni, mkutano mkuu wa TLP uliofanyika jijini Dar es Salaam ulipitisha azimio la kumuunga mkono mgombea wa CCM, Rais John Magufuli katika uchaguzi mkuu ujao.
Leave a comment