September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ofisa Takukuru ‘feki’ abambwa kwa kujipatia Sh. 90,000

Pingu

Spread the love

JAFET Emmanuel, Mkazi wa Kilimahewa katika Manispaa ya Kigoma Ujiji, anashikiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kwa kosa la kupata fedha kwa njia za udanganyifu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Kigoma … (endelea).

Taarifa iliyotolewa leo Ijumaa tarehe 5 Juni 2020 na Nestory Gatahwa, Naibu Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Kigoma imesema Emmanuel alijifanya afisa wa Takukuru kisha kutumia cheo hicho cha kughushi, kuomba fedha baadhi ya wananchi, waliokuwa wanahitaji huduma kwenye taasisi hiyo.

Katika tukio la kwanza, Emmanuel anadaiwa kuomba rushwa ya Sh. 300,000 kutoka kwa mwananchi, aliyemuahidi anaweza kutengua maamuzi ya mahakama dhidi ya shauri la mgogoro wa shamba alilokuwa nalo.

“Katika kufanikisha nia yake ovu, mtuhumiwa amejipatia Sh. 90,000 kutoka kwa mwananchi, ikiwa ni sehemu ya fedha Sh. 300,000, ambazo mtuhumiwa alimweleza mwananchi huyo ni fedha kwa ajili ya kuwezesha kutenguliwa kwa maamuzi ya mahakama katika shauri alilokuwa nalo,” inaeleza taarifa ya Gatahwa.

Tukio la pili, Emmanuel anadaiwa kuomba rushwa ya Sh. 500,000 kutoka kwa mwananchi, ili amsaidie kupata kazi katika ofisi za Takukuru. Hata hivyo, mwananchi huyo hakutoa kiasi hicho cha fedha.

Gatahwa amesema uchunguzi dhidi ya mtuhumiwa huyo unaendelea na kwamba atafikishwa mahakamani mara baada ya uchunguzi na taratibu nyingine za kisheria kukamilika.

error: Content is protected !!