Wednesday , 8 February 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Mbowe, wenzake wajifungia Zanzibar, Kina Mdee…
Habari za SiasaTangulizi

Mbowe, wenzake wajifungia Zanzibar, Kina Mdee…

Spread the love

CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), nchini Tanzania, kimejifungia Visiwani Zanzibar, kuweka mkakati wake wa kisiasa, ili kuweza kukabiliana na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake. Anaripoti Hamis Mguta, Dar es Salaam … (endelea). 

Taarifa kutoka ndani ya chama hicho zinasema, Chadema kimekwenda Zanzibar juzi Jumanne tarehe 26 Januari 2021, “kuanza kikao chake maalum (retreat)” cha siku tatu, ambacho kinalenga kupata mwelekeo wake mpya, utakaotokana na kile wanachoita, “figisu ilizokutana nazo katika uchaguzi mkuu wa 28 Oktoba 2020.”

Mkutano huo, utakaongozwa na mwenyekiti wake wa taifa, Freeman Mbowe, utajadili pia kwa kina umuhimu wa kuwapo Tume Huru ya Uchaguzi; madhara yaliyokipata chama hicho kutokana na matokeo ya uchaguzi uliopita, pamoja na mashitaka iliyowasilisha Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), iliyopo The Hague, nchini Uholanzi.

          Soma zaidi:-

Kwa mujibu taarifa iliyotumwa na katibu mkuu wa chama hicho, John Mnyika kwenda kwa wajumbe wa Kamati Kuu (CC), tarehe 22 Januari 2021, mkutano huo ulianza jana Jumatano tarehe 27 hadi kesho 29 Januari, 2021. Wajumbe walitakiwa kufika Unguja juzi jioni ya tarehe 26 Januari, 2021.

Mnyika anasema, “retreat ya Kamati Kuu itatanguliwa na Kamati Maalum ya Zanzibar ambayo itakaa tarehe 25 na 26 Januari, 2021. Baada ya hapo, vitafuata vikao vya utendaji vya Sekretariet na timu zake kwa ajili ya kukamilisha mipango iliyoamuliwa kwenye retreat ya Kamati Kuu.”

Kwa maana hiyo, Mnyika anasema, “ratiba ya retreat nzima ipo katika mtiririko huu: Tarehe 25-26 Januari, Kamati Maalum Zanzibar, tarehe 27-29 Januari, retreat ya Kamati Kuu, tarehe 30 Januari hadi tarehe 1 Februari, programming ya Sekretarieti na tarehe 2hadi 04 Februari, Compilation ya retreat itakayofanywa na timu ya Sekretarieti.

Mnyika anawaomba wajumbe kupanga mipango yao kwa kuangalia ratiba ya vikao hivyo na kuongeza wajumbe wote watarejeshewa nauli walizotumia kwa sharti la kutumia usafiri wa umma.

Aidha, mbali na kujadili mkakati na mwelekeo wake mpya wa kisiasa katika kipindi kijacho, Chadema kitautumia mkutano wa Zanzibar, kujadili jinsi ya kukabiliana na mikakati ovu inayodaiwa kupangwa na kutekelezwa na baadhi ya viongozi walioko nje ya Chadema, kwa kuwatumia waliokuwa wanachama wake 19, ambao wamefukuzwa uanachama.

Waliofukuzwa uanachama wa Chadema, ni pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake (Bawacha), Halima James Mdee; Katibu Mkuu wa baraza hilo, Grace Tendega; Makamu Mwenyekiti wa Bawacha (Bara), Hawa Subira Mwaifunga; Naibu Katibu Mkuu Bawacha (Bara), Jesca David Kishoa na aliyekuwa Katibu Mwenezi wa Bawacha, Agnesta Lambati.

Katika kikao chake cha cha dharura cha Novemba 2020, Kamati Kuu (CC) ya Chadema, ilijadili tuhuma za usaliti zilizokuwa zinawakabili viongozi hao, kisha kwa kauli moja, iliamua kumuondoa Mdee kwenye wadhifa wake wa uenyekiti wa Bawacha, na kumfuta uanachama.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana ndani ya mkutano huo, uliofanyika katika hoteli ya Bahari Beach, jijini Dar es Salaam, mbali na madai ya usaliti, Mdee na wenzake, walikabiliwa na tuhuma za kukaidi maelekezo halali ya chama chake, utovu wa nidhamu na kushirikiana na maadui wa chama.

Tuhuma nyingine,  ni pamoja na kuhujumu chama, upendeleo, kutengeneza migogoro; kughushi nyaraka na kwenda bungeni kujiapisha, kinyume na maekelezo na maamuzi ya chama chenyewe; kumsingizia mwenyekiti na kuleta taharuki kwa viongozi, wanachama na mashabiki wake.

Akizungumza kwa niaba ya wabunge wenzake, mbele ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, muda mfupi baada ya kuapishwa, Mdee alisema, amekuja kuapishwa baada ya kupata baraka kutoka chama chake.

Alisema, “tunakishukuru chama chetu cha Chadema kikiongozwa na Freeman Mbowe kwa kutupa nafasi hii. Kupitia kwao, tumepata nafasi hii ya kukiwakilisha chama chetu,” alieleza Mdee na kuongeza: “Tunawahakikishia Chadema na nchi, kwamba tutafanya kazi kwa uaminifu mkubwa.”

Kabla ya kuingia kwenye mradi wa usaliti, Mdee alijiunga na Chadema mwaka 2004 na mara moja akabahatika kuwa mbunge wa Viti Maalum, kutoka mwaka 2005 hadi 2010 na baadaye akawa mbunge wa Kawe kati ya mwaka 2010 hadi Juni 2020.

Wengine waliofukuzwa uanachama na ambao kikao hicho kitajadili ushiriki wao katika  kuhujumu chama na hivyo, kuweka mkakati wa kukinusuru, ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoani Mtwara, Tunza Malapo; aliyekuwa Naibu Katibu mkuu wa Bawacha Zanzibar, Asia Mwadin Mohamed; Cecilia Pareso, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Salome Makamba,  Anatropia Theonest, Conchesta Lwamlaza, Felister Njau na Stella Siyao.

Vyanzo vya taarifa vinasema, mkutano wa Zanzibar (retreat), utajadili ushiriki wa baadhi ya viongozi wandamizi wa chama hicho, wakiwamo wakurugenzi wake wawili, wanaodaiwa kusaidiana na Mdee na Tendega, kufanikisha mpango huo haramu wa kughushi nyaraka za chama na kisha kuwasilisha orodha ya majina ya wabunge wa Viti Maalum,  Tume ya taifa ya uchaguzi (NEC).

MwanaHALISI Online limeelezwa orodha ya majina ya wanawake waliotangazwa kuwa wabunge wa Viti Maalum, iliwasilishwa NEC na Mdee – “mwanachama wa hiari wa Chadema,” na wenzake watatu, akiwamo Tendega, kwa msaada kutoka kwa baadhi ya wanachama wa CCM ambao walipata kuwa Chadema.

“Hiki chama kimejengwa kwa jasho na damu. Hiki chama kimebeba matumaini ya mamilioni ya Watanzania. Hiki chama siyo mali ya Mbowe. Ni mali ya wananchi wote katika Jamhuri ya Muungano. Hivyo basi, tunakwenda Zanzibar kujisuka upya,” ameeleza mmoja wa wajumbe wa Kamati Kuu kwa sharti la kutotajwa jina gazetini.

Amesema, Watanzania wana matumaini makubwa na Chadema, hivyo ni lazima tumaini hilo liheshimiwe na sisi viongozi kwa kutengeneza mkakati wa kudumu wa kukabiliana na CCM na kukilinda chama hiki na maadui zake wa ndani na nje.

“Mbali na kujadili mwelekeo wa chama katika siku zijazo, tunakwenda kujadili jinsi ya kumalizana na kina Mdee kwenye Baraza Kuu (BKT), ambako wamewasilisha rufaa yao, kupinga maamuzi ya Kamati Kuu ya kuwavua uanachama.

“Hakuna shaka kuwa tutakapokutana, tutaweka msimamo wa pamoja wa kusimamia kile tulichokiamua kwenye Kamati Kuu. Hatuwezi kukubali kusalitiwa na watu ambao tuliwapa dhamana,” ameeleza kiongozi huyo mwandamizi ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini.

MwanaHALISI Online limeelezwa mkutano wa Zanzibar (retreat), utakaohudhuriwa na aliyekuwa mgombea wake wa urais, Tundu Antipas Lissu, utapokea taarifa rasmi ya kinachoendelea kwenye malalamiko yake iliyowasilisha mjini The Hague.

Taarifa ya malalamiko yaliyowasilishwa The Hague, itawasilishwa kwenye kikao hicho na Lissu, ambaye atashiriki mkusanyiko huo kwa njia ya mtandao, kutokea nchini Ubelgiji alikokwenda baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020.

Chadema kinadai kimewasilisha malalamiko yake The Hague, kufuatia kuwapo kwa vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu, ikiwamo kutumbukia katika utawala wa kimabavu katika kipindi cha miaka mitano ya ukandamizaji, utekaji na utumiaji wa nguvu uliopitiliza dhidi ya wagombea wa upinzani na viongozi wake.

Chadema kimekuwa kikidai matokeo ya uchaguzi huo, yalikuwa yanaingia kuwa “haramu,” na kuomba jamii ya kimataifa kutoyatambua, na kuongeza kuwa “kilichotokea siyo uchaguzi bali udanganyifu usio kifani.”

Hata hivyo, madai hayo yamekanushwa vikali na Mwenyekiti wa Tume ya taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mstaafu Semistocles Kaijage pamoja na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro, ambaye alieleza wanaoeneza taarifa hizo, wanalengo la kuichafua serikali mbele ya jumuiya za kimataifa.

Katika uchaguzi huo wa tarehe 28 Oktoba 2020, Chadema kiliambulia kiti kimoja pekee cha ubunge, katika jimbo la Nkasi Kaskazini, mkoani Rukwa, kutoka viti 36 vya majimbo ilivyopata katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Kwa upande wa viti Maalum, chama hicho kimepata viti 19, ukilinganisha na viti 35 ilivyopata mwaka 2015, ambavyo inadai kutovitambua kutokana na kile inachosema, “uchaguzi wa mwaka jana ulivurugwa kwa kiwango kikubwa na mamlaka zinazousimamia.”

Vile vile, mkutano wa Zanzibar, utakaowakutanisha viongozi kadhaa wa chama hicho, wakiwamo wajumbe wote wa Kamati Kuu (CC), pamoja na wataalam mbalimbali, unatarajia kuivunja sektarieti ya Kamati Kuu iliyopo sasa na kuunda sekretarieti mpya itakayokuwa na uwezo wa kusimamia maamuzi, maelekezo na mikakati itakayopitishwa.

“Suala la uvunjaji wa sekretarieti ya chama, hili halina mjadala. Tayari mapendekezo yako mezani kwa mwenyekiti na wakurugenzi wote wanaofanya kazi makao makuu, ambao ndio wajumbe wa sekretarieti mikataba yao imevunjwa tokea Desemba mwaka jana. Kwa msingi huo, tutakaporudi Zanzibar, tunategemea kutangazwa kwa sekretarieti mpya,” ameeleza kiongozi mwingine wa Chadema, ambaye yuko karibu na Mbowe.

Kwa mujibu wa Katiba ya Chadema, Sekretarieti ya chama hicho, inaundwa na mwenyekiti wake kwa kushirikiana na Katibu Mkuu; kazi ya Kamati Kuu ni kuidhinidha mapendekezo hayo.

Chadema inakutana Zanzibar ikiwa imegoma kutambua matokeo ya uchaguzi uliyopita, ikiwa pamoja na kutotambua nafasi za wabunge wa Viti Maalum na ruzuku, jambo ambalo litawalazimu kutafuta njia mbadala ya kuweza kulipa watumishi wake, watakaohudumu makao makuu Kinondoni na ofisi zake 10 za kanda.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Bunge labaini madudu mfumo ukusanyaji mapato, h’shauri tatu kikaangoni

Spread the love  KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali...

Habari za Siasa

Mkuu wa wilaya ya Rungwe azindua vyumba sita vya madarasa vya thamani ya 64 mil

Spread the love  MKUU wa Wilaya ya Rungwe, Jaffar Haniu amezindua vyumba...

Habari za Siasa

Mbunge afurahia mabilioni ya Samia kutua jimboni

Spread the love  MBUNGE wa Igunga, Nicholas Ngassa ameishukuru Serikali kwa utekelezaji...

Habari za Siasa

PIC yaishauri Serikali kuanzisha mfuko wa uwekezaji kusaidia mashirika ya umma

Spread the love  KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji...

error: Content is protected !!