July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kina Mdee waanzisha vita mpya Chadema

Spread the love

HATUA ya Halima James Mdee na wenzake 18, kushitaki Kamati Kuu (CC) ya (Chadema, mbele ya Baraza Kuu la taifa (BKT), yaweza kuwa mwisho wa kundi hilo kisiasa. Anaripoti Kelvin Mwaipunga, Dar es Salaam … (endelea).

Taarifa kutoka kwa watu mbalimbali zinasema, uamuzi wa Mdee na wenzake, kukimbilia kamati kuu, kutawafanya viongozi wakuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, kupambana ili kuhakikisha maamuzi yao, yanasimama kama yalivyo.

“Huu ni mgogoro mwingine mkubwa ambao Mdee na wenzake, wameamua kuutafuta,”ameeleza mmoja wa wajumbe wa CC ambaye hakupenda kutajwa na kuongeza, “hakuna namna ambayo mwenyekiti wa chama na Kamati Kuu yake, wanaweza kurudi nyuma, kutotetea maamuzi yao.”

Anasema, “hii ni kwa sababu, ikiwa mwenyekiti atashindwa katika shauri hili, maana yake ni kuwa Mdee na wenzake, wananguvu kuliko mwenyekiti wa kamati kuu, Freeman Mbowe na wajumbe wenzake.”

Mdee na wenzake 18, wameripotiwa na vyombo vya habari, kuandika barua za kupinga uamuzi wa kuwavua uachama wa chama hicho, uliofanywa na Kamati Kuu, tarehe 27 Novemba mwaka huu.

Katika sakata hilo, Mdee na wenzake, walituhumiwa na kutiwa hatiani kwa makosa ya utovu wa nidhani, unasaliti, upendeleo, kutengeneza makundi na kushirikiana na wanaokitakia mabaya chama.

Tuhuma nyingine zilikuwa kujipeleka bungeni jijini Dodoma na kuapishwa na Spika Job Ndugai, kuwa wabunge wa viti maalum, kinyume na maelekezo na katiba ya chama.

Akitangaza uamuzi huo, Mbowe alisema,  Mdee ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa chama hicho (Bawacha) na wenzake, walikuwa na fursa ya kukata rufaa Baraza Kuu, ndani ya siku 30 tangu kutolewa kwa adhabu hiyo.

Muda huo wa siku 30, ulihitimishwa jana Jumapili saa 11 jioni kwa Mdee na wenzake 18 kuwasilisha rufaa za kupinga uamuzi huo wa Kamati Kuu, iliyokuwa ikiongozwa na Mbowe.

Uamuzi huo wa Mdee na wenzake, ni ishara kwamba wameanzisha vita mpya kwani kinachofanyika sasa ni Kamati Kuu yote inayoongozwa na Mbowe imeshtakiwa Baraza Kuu.

Kitakachokwenda kufanyika katika mkutano huo wa Baraza Kuu ambao haujafahamika utaitishwa lini, ni Kamati Kuu kwenda mbele ya Baraza Kuu kutetea uamuzi walioufanya huku Mdee na wenzake 18 wakiingia kuwashawishi wajumbe wa mkutano huo zaidi ya 600 kuwarejeshea uanachama wao.

Duru za siasa, zinatizama hatua hiyo kama vita mpya ya kamati kuu na Mdee na wenzake 18 kwani ikitokea wakashinda, itakuwa ina maanisha Mbowe na kamati kuu yake itabidi ijitafakari na huenda ikazua joto kali za mabadiliko ya kiuongozi.

MwanaHALISI Online limeelezwa kuwa watuhumiwa wote 19, wakiwamo waliokuwa viongozi waandamizi wa Chadema, wamewasilisha rufaa zao, ofisini kwa katibu mkuu wa chama hicho, John Mnyika.

Mbali na Mdee, wengine waliofukuzwa Chadema, ni waliokuwa wajumbe wa CC, Ester Bulaya na Esther Matiko; aliyekuwa katibu mkuu wa Baraza la Vijana la chama hicho (Bavicha), Nusrat Hanje; aliyekuwa katibu Mkuu Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Grace Tendega na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti Bawacha (Bara), Hawa Subira Mwaifunga.

Wapo pia, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Bawacha Bara, Jesca David Kishoa; aliyekuwa katibu mwenezi wa Bawacha, Agnesta Lambat; aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema mkoani Mtwara, Tunza Malapo na aliyekuwa naibu katibu mkuu wa Bawacha Zanzibar, Asia Mwadin Mohamed.

Katika orodha hiyo, yupo pia aliyekuwa mbunge wa Viti Maalum katika Bunge lililopita, kutoka mkoani Arusha, Ceciia Pareso; aliyekuwa mbunge wa Same Mashariki,  Naghenjwa Kaboyoka; aliyekuwa mbunge wa viti maalum mkoani Mbeya, Sophia Mwakagenda na aliyekuwa mbunge wa viti maalum mkoani Dodoma, Kunti Majala.

Wengine, ni aliyekuwa mbunge wa viti maalum mkoani Shinyanga, Salome Makamba; aliyekuwa mbunge wa viti maalum mkoani Dar es Salaam,  Anatropia Theonest; aliyekuwa mbunge wa viti maalum mkoani Kagera,  Conchesta Lwamlaza; na wanachama wengine wawili, Felister Njau na Stella Siyao.

error: Content is protected !!