May 21, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Taifa Stars ‘out’ CHAN

Spread the love

 

TIMU ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars ) imeondolewa kwenye michuano ya Kombe la Mataifa Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Guinea. Anaripoti Kelvin Mwaipungu, Dar es Sakaam … (endelea).

Stars iliyokuwa kwenye kundi D, kwenye michuano hiyo imeshindwa kupita kwenye hatua ya robo fainali baada ya kumaliza kwenye nafasi ya tatu ikiwa na pointi nne.

Kwenye mchezo huo Guinea ilikuwa ya kwanza kupata bao kwa njia ya penalti dakika ya 5 kupitia kwa Yakhouba Bally baada ya mlinzi wa Taifa Stars kushika mpira katika eneo la hatari.

Dakika 13, baadae Baraka Majogoro alisawazisha bao hilo kwa shuti kali na kufanya timu hizo kwenda mapumziko zikiwa zimefungana bao 1-1.

Kipindi cha pili kilianza kwa Taifa Stars kushambulia kwa nguvu na kufanikiwa kupachika bao la pili kwa njia ya kona kupitia kwa Edward Manyama aliyeunganisha kwa kichwa kona ya Farid Mussa dakika ya 68 ya mchezo.

Mara baada ya kupata bao hilo Taifa Stars ilijikuta kwenye wakati mgumu kutokana na kushambuliwa na Guinea na hatimaye dakika ya 82 walisawazisha bao hilo kupitia kwa Victor Kantabadouno na kufanya mechi hiyo kumalizika kwa sare na kila timu kuondoka na pointi moja.

Hii itakuwa ni mara ya pili kwa Taifa Stars kushindwa kuvuka kwenye hatua ya makundi kama ilivyokuwa mwaka 2009 kwenye michuano kama hii na kushika mafasi ya tatu, wakati huo timu ilikuwa chini ya kocha Marcio Maximo.

error: Content is protected !!