May 29, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbowe apata pigo jingine, ampoteza mama mkwe

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema

Spread the love

 

FREEMAN Mbowe, kiongozi wa chama kikuu cha upinzani Tanzania cha Chadema ameendelea kuandamwa na majanga baada ya kumpoteza mama mkwe wake, Johara Mtei (79). Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Johara amefikwa n amauti leo Ijumaa tarehe 20 Agosti 2021 katika Hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam, alipokuwa amelazwa kwa matibabu.

Marehemu Johara ni mke wa Edwin Mtei, mwasisi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambaye pia amewahi kuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Mtei alikuwa Gavana wa kwanza wa Benki Kuu kati ya Juni 1966 hadi Januari 1974 katika utawala wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Msiba huo umetokea ikiwa ni siku 28 zimepita tangu Mbowe alipompoteza baba yake mdogo, Manase Alphayo Mbowe.

Johari Mtei

Manase alifikwa na mauti tarehe 23 Julai 2021, katika Hospitali ya Machame mkoani Kilimanjaro, alikokuwa anapatiwa matibabu baada ya kusikia taarifa za mwanae huyo Mbowe kufunguliwa kesi ya ugaidi.

Mbowe amemuoa Dk. Lilian, ambaye ni binti wa Edwin Mtei na marehemu Johara.

Mashinda Mtei, mtoto wa Edwin Mtei amesema, ni kweli mama yao amefariki na kwa sasa wanaelekea mkoani Arusha kutoka Dar es Salaam kwa ajili ya maandalizi ya maziko.

Mbowe ambaye yuko mahabusu kwenye kuta nne za Gereza Kuu la Ukonga jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za uhujumu uchumi na kupanga njama ya ugaidi kwa zaidi ya mwezi sasa.

Vifo hivyo vyote vimetokea yeye akiwa gerezani ambapo kifo cha Manase hakuhudhuria msiba sanjali na huu wa mama mkwe wake.

Huu ni msiba wa tatu kumkuta Mbowe ndani ya wiki chache, baada ya kaka yake, Charles Mbowe, kufariki dunia, tarehe 8 Julai 2021, na mwili wake kuzikwa nyumbani kwao Machame mkoani Kilimanjaro, tarehe 12 Julai 2021.

Edwin Mtei

Viongozi mbalimbali wametuma salamu za rambirambi kupitia kurasa zao za kijamii akiwemo Katibu Mkuu wa Chadema, John John Mnyika ameandika “nimepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Johari Mtei-Mke wa Mzee Edwin Mtei Mwenyekiti muasisi wa Chadema. Poleni sana familia na ukoo kwa msiba. Tumweke Mzee Mtei kwenye maombi katika kipindi kigumu ambayo yeye na familia wanapitia.”

Naye Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe ameandika “nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Mama Johara Mtei, Mke wa Mzee Edwin Mtei (muasisi wa
Chadema na mkwe wa kaka Freeman Mbowe, mwenyekiti wa Chadema.

Pole nyingi kwa Mzee Mtei, Dk. Lillian Mtei, Mashinda Mtei na watoto wote. Mola ampumzishe Mama mahala pema peponi.”

error: Content is protected !!