MWENYEKITI wa Chama cha Maendeleo na Demokrasia (Chadema), Freeman Mbowe, ameiomba Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, ifanyie kazi hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ), inayoitaka irekebishe vifungu vya Sheria ya Vyama vya Siasa, vinavyokwenda kinyume na mtakaba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Anaripoti Mwandishi Wetu, Arusha … (endelea).
Mbowe ametoa wito huo leo Ijumaa, tarehe 25 Machi 2022 jijini Arusha, muda mfupi baada ya mahakama hiyo kutoa hukumu wa kesi namba 3/2020, iliyofunguliwa na viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani Tanzania, kwa kushirikiana na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kuipinga sheria hiyo.
“Na kipekee namtaka Rais Samia aone kwamba sheria yetu ya vyama vya siasa tayari inanyooshewa vidole na majaji wote wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, hili ni jambo la msingi sana. Natambua pamekuwa na malalamiko mengi na hata ndani wenyewe marekebisho ya baadhi ya sheria yameanza kufanyika,” amesema Mbowe.
Mbowe amesema, “marekebisho hayo bado hayajafikia ukomo, ila ninachokisema Serikali ijitahidi kadiri iwezekanavyo turekebishe sheria zetu, tufanye nchi yetu mahali salama pa kufanya siasa, kushauriana, kuwa na uhuru wa watu na haki ziweze kudumishwa.”
Aidha, Mbowe amelishukuru Jopo la Majaji wa EACJ walitoa hukumu hiyo, akiwemo jaji Charles Nyachae, akisema uamuzi wao utawajengea mazingira rahisi kwa wao kufanya siasa za demokrasia nchini.
Kesi hiyo ilifunguliwa na viongozi wa vyama vya siasa, akiwemo Mbowe, kupinga sheria hiyo kwa madai inampa mamlaka Msajili wa Vyama vya Siasa nchini.
Wengine waliofungua keai hiyo ni, Hayati Maalim Seif Shariff Hamad; Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe na Mwenyekiti wa Chama cha CHAUMMA, Hashim Rungwe.
Katika kesi hiyo, kina Mbowe walikuwa wanapinga vipengele vya sheria ya vyama vya siasa, ikiwemo kifungu kinachompa Msajili wa vyama vya siasa, mamlaka ya kuingilia wakati wowote shughuli za chama cha siasa.
Vifungu vingine vilivyopingwa ni kile kinachompa msajili wa vyama vya siasa, mamlaka ya kuingilia uongozi wa chama cha siasa na kumsimamisha uanachama mwanachama yeyote kushiriki shughuli za kisiasa.
Walidai Vifungu vyote hivyo vinakiuka misingi ya utawala bora na kidemokrasia, pamoja na mkataba wa EAC.
Leave a comment