November 30, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbatia atimuliwa, Selasini Makamu Mwenyekiti mpya NCCR Mageuzi

Joseph Selasini (kulia) na James Mbatia

Spread the love

MKUTANO Mkuu wa dharura wa Chama cha NCCR -Mageuzi uliofanyika leo tarehe 24 Septemba, 2022 umemtimua aliyekuwa mwenyekiti wa Chama hicho, James Mbatia kwa kumvua wadhifa wake pamoja na uanachama wa chama hicho.

Pia aliyekuwa Naibu katibu mkuu wa chama hicho, Angelina Mutahiwa naye amevuliwa wadhifa huo pamoja na uanachama. Viongozi hao wote kwa pamoja wanadaiwa kuchukuliwa hatua hizo kutokana na utovu wa nidhamu. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma… (endelea)

Miongoni mwa tuhuma hizo Mbatia ni kuuza mali za chama, ikiwemo mashamba na nyumba katika maeneo mbalimbali.

Mkutano huo umefanyika leo jijini Dodoma na kuhudhuriwa na wajumbe 224 kati ya 368 waliopo kwa mujibu wa Katiba ya chama chao.

Wajumbe hao walichukua uamuzi huo baada ya Kaimu Mwenyekiti wa chama hicho, Haji Ambari Hassan kuorodhesha tuhuma saba zinazomkabili Mbatia na tuhuma mbili za Angelina.

Amewaeleza wajumbe hao kuwa viongozi hao walipelekewa hati ya mashtaka yao na walitakiwa kujibu ndani ya siku 14 kama katiba yao inavyotaka.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia akisalimiana na Joseph Selasini kabla ya kumkabidhi kadi ya NCCR-Mageuzi katika kikao cha watia nia wa Ubunge kilichofanyika jijini Dodoma tarehe 27 Juni, 2020.

Amesema watuhumiwa hao hawakujibu mashtaka hayo na wala hawakufika katika mkutano huo  licha ya kualikwa ili wajitetea mbele ya wajumbe.

Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini ya chama hicho Joseph Selasini ambaye amechaguliwa kuwa makamu mwenyekiti wa chama hicho, amesema mkutano huo kwa pamoja pia umewafukuza uanachama wanachama 10 kwa utovu wa nidhamu uliokidhiri akiwemo Edward Simbeye.

Amesema baadhi ya wanachama ambao walikuwa wakikitukana chama kwenye mitandao pamoja na kuitisha mikutano na vyombo vya habari.

Katika uchaguzi huo, Selasini amepata kura 173 kati ya 232 zilizopigwa katika uchaguzi huo, huku mshindani wake Jerehemiah Maganga akipata kura 59.

Selasini ameeleza kuwa mkutano huo pia umeweka maazimio ya ukomo wa mwenyekiti ambapo kwa sasa atakuwa anaongoza kwa kwa miaka mitano na akimaliza anaweza kutetea nafasi yake vivyo hivyo kwa nafasi ya uenyekiti hatozidi kipindi cha miaka 10.

Aidha, ameeleza kuwa wameazimia kufanya mabadiliko ya katiba na kuwapa nafasi makatibu wa mikoa kuwa wajumbe wa mkutamo mkuu wa chama hicho.

Sambamba na hilo Selasini ameeleza kuwa pia makatibu wa wilaya nao watakuwa wajumbe wa mkutano mkuu wa mkutano huo tofauti na ilivyo sasa.

error: Content is protected !!