Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limefunga kipande cha njia cha ‘ARROW GLACIER” ambacho hutumika na baadhi ya wageni wanaopanda mlima Kilimanjaro kupitia njia ya Machame, Umbwe, Lemosho na Londorosi kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).
Mvua hizo kwa mwaka huu zimekuwa kubwa kuliko ilivyozoeleka na kusababisha maporomoko ya mawe, miamba ya barafu na utelezi na hivyo kuwa hatari kwa watumiaji wa njia hiyo.
Taarifa iliyotolewa leo Jumamosi na Afisa Uhifadhi Mwandamizi Kitengo cha Mawasiliano-TANAPA Catherine Mbena imesema ukaguzi uliofanywa na timu ya wataalam ya Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro ikishirikiana na wataalamu wa taasisi ya NOLS (National Outdoor Leadership School) wenye uzoefu katika masuala ya usalama mlimani, umeonyesha kuwa hali imezidi kuwa mbaya.
Amesema maporomoko ya mawe, miamba ya barafu na utelezi yameongezeka na kwamba kwa sasa si salama kwa watumiaji.
“TANAPA inasitisha matumizi ya kipande hicho cha njia na badala yake itumike njia ya kawaida ya kutokea Baranco kuelekea Karanga na Barafu hadi kufika kileleni mpaka pale mvua zinazoendelea kunyesha zitakapokoma na kufanyika ukaguzi kujiridhisha kuwa njia hiyo ni salama kwa wapanda mlima na watoa huduma mlimani.
“Kipande cha “ARROW GLACIER” kinaanzia karibu na kituo cha Baranco katika eneo la “LAVA TOWER” na kinapita kwenye kasoko (crater) kuelekea kileleni ambapo wageni hupendelea kupita eneo hilo kwa ajili ya kuona mandhari nzuri ya mlima na pia ni rahisi kwa wageni kufika kileleni,” amesema.
Leave a comment